Saturday, 30 July 2016

USIMAMIZI WA RUTUBA YA UDONGO KATIKA KUONGEZA UZALISHAJI WA MAZAO


Engineer Octavian Lasway,kwa msaada wa mtandao na TOAM(tanzania organic agriculture movement) 
Sehemu ya 01
Malengo ya makala hii kwa mkulima

  •   Kufahamu aina za udongo zilizopo na sifa zake.
  •  Kuelewa kwamba kudhibiti rutuba ya udongo hakuishii katika kuongeza mbolea au kuongeza mavuno peke yake. Kwanza, inajumuisha kulinda udongo na kuongeza mboji pia na shughuli za vijidudu ndani yake ili kuzuia kupotea kwa udongo na kuhimiza virutubisho vya kutosha, maji na afya ya mimea, kuongeza na kupata mavuno ya kutosha wakati wote.
  •  Kufahamu zana za udhibiti wa rutuba ya udongo na kuweza kuziunganisha katika njia stahiki ili ziendane na mazingira ya shambani na mahitaji ya mazao.
 Utangulizi

 Wasiwasi unatanda kuhusu uendelevu wa muda mrefu wa sekta ya kilimo. Ardhi yenye rutuba na maji ya kutosha ni muhimu kwa ajili ya kuendeleza kilimo na kaya. Hata hivyo, katika bara la Afrika uzalishaji unaotokana na ardhi umekuwa ukiendelea kupungua kutokana na shughuli za kilimo kilichoshadidi zinazosababisha uharibifu wa ardhi. Sababu kubwa za uharibifu wa ardhi ni taratibu za kilimo zisizokuwa endelevu kama vile kulima kwenye miteremko mikali bila ya kuchukua hatua za kuhifadhi udongo na maji, kulima zao la aina moja tu, utifuaji wa ardhi uliopitiliza, kupungua kwa mazoea ya kupumzisha ardhi bila ya kuchukua hatua stahiki za kurudishia virutubisho vya ardhi, kuchoma mabaki ya mazao, kugeuza misitu na vichaka kuwa maeneo ya kilimo cha kudumu, au matumizi yaliyopitiliza ya misitu kwa ajili ya kuvuna kuni na mbao, mifugo mingi katika eneo dogo la malisho, na kutokuwepo kwa udhibiti imara wa mboji kwenye udongo.

Uharibifu wa ardhi hutokea katika aina tofauti katika matumizi mbalimbali ya ardhi:

  • Shambani, mmomonyoko wa udongo hutokea kupitia: maji na upepo; uharibifu wa kikemikali  hii inasababishwa na waakulima wengi kutumia mbolea za viwandani bila ushauri au maelezo kutoka kwa wataalamu ili wamwabie mbolea sahihi kwa ajili ya udongo wake kwa zao analolima – kwa sehemu kubwa ni kupungua kwa rutuba – kutokana na virutubisho kuchuja; uharibu wa udongo wa kimaumbile kutokana na mgandamizo, kufunikwa na kuondolewa tabaka la juu; uharibifu wa kibiolojia kutokana na kukosekana kwa miti au majani ya kuufunika, kupungua kwa mboji ardhini; uharibifu unaotokana na maji unaosababishwa na kuongezeka kwa kasi ya maji (kuchafua maji ya juu) na kupungua kwa maji kutokana na upotevu kupitia kiwango cha juu cha mvukizo
  • Katika ardhi ya malisho, uharibifu wa kibiolojia hutokea kupitia kupotea kwa miti na majani yanayofunika udongo na spishi zenye faida. Matokeo yake, spishi za kigeni na ‘zisizotakiwa’ huvamia ardhi. Uharibifu wa kimaumbile husababisha kasi kubwa ya maji juu ya ardhi na mmomonyoko. Kwa kigezo cha eneo lililoathiriwa, inakadiriwa kwamba mifugo mingi katika eneo dogo ndio sababu kubwa muhimu zaidi inayochangia uharibifu wa ardhi, ikifuatiwa na mbinu duni za kilimo na kilimo shadidifu hasa katika mikoa ya wafugaji kama Arusha, Manyara, Shinyanga n.k
  • Kwa hiyo juhudi za kupunguza njaa katika Nchi yetu lazima zianzie kwa kushughulikia udongo wake ambao umechoka kwa kiasi kikubwa; kuongeza na kupanua wigo wa matumizi ya ardhi ikijumuisha matumizi ya mbinu za usimamizi wa rutuba ya udongo zinazojikita katika kudhibiti mmomonyoko wa udongo, kulinda ardhi, kudhibiti mboji kwenye udongo, kupunguza utifuaji wa ardhi, na matumizi stahiki ya virutubisho, mbolea na umwagiliaji. Matumizi ya mbegu bora, na maboresho katika upatikanaji wa pembejeo na masoko ya chakula pia huchangia katika kuongeza tija kwa kiwango kikubwa na kuendeleza uzalishaji wa chakula kwa ujumla ndani ya kaya na taifa kwa ujumla, pia hii itachangia katika kuinua kipato kwani kilimo ni biashara na tayari kimeajiri vijana wengi, kwa hiyo kupima na kuelewa vizuri kuhusu udongo ambao ndio hubeba chakula cha mimea ni chanzo cha mkulima kupata faida

 UDONGO

 Udongo ni nini?

‘Udongo’ ni tabaka juu ya ardhi ambalo hufanya kazi kama chombo cha kukuzia mimea. Udongo hujengwa kutokana na shughuli zinazoendelea za hali ya hewa kulingana na vipengele kadhaa vya mazingira. Kwa sehemu kubwa kuundwa kwa udongo hutawaliwa na vipengele vikuu vitano: hali ya nchi (k.m. mvua, joto na upepo), mwinuko wa eneo (mahali eneo lilipo), viumbe hai (mimea na vijidudu), asili ya kitu kilichozalisha udongo (aina ya miamba na madini ambayo udongo unatokananayo) na muda. 

 Udongo umetengenezwa na nini na unafanya nini?

 Vitu vya msingi vinavyotengeneza udongo ni madini, mabaki ya viumbe hai, maji na hewa. Udongo unaofaa (unaofaa kwa ajili ya kukuza mimea mingi) huundwa kwa asilimia takribani 45% ya madini, maji 25 %, hewa 25 %, na mabaki ya viumbe hai 5 %. Katika hali halisi, asilimia hizi za sehemu nne hutofautiana sana kutegemea vipengele vingi kama vile hali ya nchi, upatikanaji wa maji, mbinu za kilimo na aina ya udongo. Hewa na maji kwenye udongo hupatikana katika nafasi za matundu kati ya punje za udongo. Uwiano kati ya nafasi ya tundu lililojaa hewa na tundu lillilojaa maji mara nyingi hubadilika kila msimu, wiki na hata kila siku, kutegemea maji yanayoongezeka kupitia mvua, mtiririko, maji ya ardhini na mafuriko. Ukubwa wa tundu lenyewe huweza kubadilika, kwa namna yoyote ile, kupitia michakato mbalimbali. Mabaki ya viumbe hai kwa kawaida huwa chini zaidi ya 5 % katika aina mbalimbali za udongo ambao hausimamiwi vyema. 

Sehemu ya Madini

Sehemu ya madini katika udongo imegawanywa katika aina tatu kulingana na ukubwa wa punje: mchanga, mchangatope na mfi nyanzi. Mchanga, mchangatope, na mfi nyanzi kwa pamoja hujulikana kama sehemu ya udongo yenye punje ndogo. Punje hizo zina kipenyo cha chini ya 2mm . Punje kubwa za udongo hujulikana kama vipande vinavyotokana na miamba, pia vina ukubwa tofauti (changarawe, mawe na jabali). Uwiano huu uliopo wa mchanga, mchangatope na mfinyanzi hujulikana kama ‘umbile asili’ la udongo. Umbile asili la udongo lina jukumu muhimu katika mfumo wa matumizi ya virutubisho kwa sababu lina uwezo wa kufanya virutubisho na maji kubaki au kutokubaki kwenye udongo. Kwa mfano, udongo wenye umbile asilia laini una uwezo mkubwa wa kuhifadhi virutubisho vya udongo. Udongo wenye umbile asilia laini huitwa udongo wa mfinyanzi, wakati udongo wenye umbile asilia lenye chenga chenga huitwa mchanga. Hata hivyo, udongo ulio na mchanganyiko sawa wa mchanga, mchangatope na ufinyanzi na kuonyesha tabia ya kila moja, huitwa ‘udongo tifutifu’ wenye rutuba

Maji ya Udongo

Virutubisho vyote kwenye udongo vinavyoingia kwenye mmea vinatokana na maji yaliyopo kwenye udongo. Kwa njia muhimu zaidi, maji huamua iwapo udongo utakuwa na rutuba iliyotarajiwa pia na lishe ya mmea. Ni kiasi kidogo tu cha maji kinahitajika kuruhusu udongo kuwa na hewa. Kama maji ni mengi kwenye udongo na kama yatabaki kwa siku nyingi – ikimaanisha udongo umejaa maji – udongo utaishiwa oksijeni. Katika mazingira haya, virutubisho vya mmea havitapatikana kwa mimea, na vijidudu vingi vyenye manufaa kwenye udongo havitaishi. Mimea mingi itakufa katika mazingira kama haya, isipokuwa mimea michache kama vile mpunga na magimbi. Kazi kubwa ya maji katika udongo ni:
a) Kukuza shughuli za udongo za kimaumbile na kibiolojia
 b) Hufanya kazi kama kiyeyushi na kisafirishi cha virutubisho
 c) Hufanya kazi kama wakala katika mchakato wa mimea kutengeneza chakula kutokana na mwanga ‘fotosinthesisi’
 d) Hufanya kazi yenyewe kama kirutubisho
e) Hufanya mimea kututumka na kuwa migumu(turgidity)
f) Hufanya kazi kama wakala wakati miamba na madini inapo momonyolewa na hali ya nchi.


Hewa ya udongo

Oksijeni ni muhimu kwa michakato yote ya kibiolojia inayotokea kwenye udongo. Hupatikana kwa vijidudu na mizizi ya mimea kupitia nafasi kubwa na ndogo kwenye udongo.

Mboji ya udongo

 Mabaki ya viumbe hai katika udongo, ambayo hujulikana kama sehemu ya udongo inayoitwa mboji, inaweza kugawanywa katika sehemu kuu tatu: vijidudu ambavyo bado viko hai, mabaki ambayo hayajaoza au yaliyooza kidogo, na mabaki yaliyooza kabisa. Mboji ni mabaki ya viumbe hai yaliyooza vizuri na hayabadiliki kabisa. Mboji kwa sehemu kubwa hupatikana katika tabaka la juu la udongo, mahali ambapo kuna shughuli nyingi za kibiolojia zinazoendelea. Mabaki ya viumbe hai kwenye udongo yanayoozeshwa na vijidudu vya kwenye udongo, huweza kuungana na punje za udongo zenye asili ya madini na kutengeneza punje imara za mboji zinazoweza kubaki kwenye udongo kwa miaka mingi. Punje au mboji hii ya muda mrefu huchangia kwa sehemu kubwa kuboresha muundo wa udongo. Mboji hutengeneza kuanzia Udongo wenye zaidi ya asilimia 12 hadi 18 ya kaboni inayotokana na viumbe hai (takribani asilimia 20 hadi 30 ya mboji) huitwa udongo wa mboji. Kuna faida nyingi ya kuwa na kiwango cha juu cha mboji isiyobadilika kwa urahisi katika udongo unaotumika kwa kilimo.

Faida hizi zinaweza kuwekwa katika makundi matatu:

 a) Faida za kimaumbile: Mboji ya udongo hukuza uthabiti wa punje za udongo, huboresha upenyaji wa maji na mzunguko wa hewa kwenye udongo, hupunguza kasi ya maji juu ya ardhi, huboresha uwezo wa udongo kuhodhi maji; hupunguza mnato wa udongo wa mfinyanzi na kufanya iwe rahisi kulimwa; kupunguza tabaka la juu la udongo kukauka, na huwezesha matayarisho ya vitalu. 
b) Faida za kikemikali: Mboji ya udongo huongeza uwezo wa udongo wa kuhodhi na kuipatia mimea virutubisho muhimu kwa muda mrefu, kama vile kalsiam, magnesia na potasiam, ambazo pia hufahamika kama ‘Uwezo wa Mabadiliko ya Kikemikali’ (CEC); huboresha uwezo wa udongo wa kumudu mabadiliko ya pH (kipimo cha asidi) – hii pia hujulikana kama uwezo wa kinga; huharakisha kuoza kwa madini kwenye udongo kwa muda mrefu, na hufanya virutubisho vilivyoko kwenye udongo viweze kupatikana na kutumika na mimea.
 c) Faida za kibiolojia: Mboji ya udongo huvipatia chakula viumbe hai kwenye udongo; hukuza bioanuwai na shughuli za vidudu kwenye udongo, ambayo huweza kusaidia kuzuia magonjwa na wadudu waharibifu wa mazao; na hukuza nafasi kwenye matundu ya udongo kupitia shughuli za vijidudu vya udongo. Hii husaidia kuongeza upenyaji katika udongo na kupunguza kasi ya maji juu ya ardhi. 

Vidudu na vijidudu vya udongo

 Udongo pia ni mahali panapoishi viumbe wengi, baadhi yao huonekana kwa macho kama vile minyoo ya ardhini na mchwa. Wengine ni wadogo sana na huweza kuonekana chini ya darubini peke yake, hivi ni vijidudu. Miongoni mwa vidudu muhimu sana vya udongo ni minyoo ya ardhini na mchwa. Wakulima wengi wanafahamu kwamba kuwepo kwa minyoo ni dalili ya udongo wenye rutuba. Minyoo hutekeleza kazi nyingi muhimu: Kwanza huharakisha kuoza kwa mabaki ya mimea juu ya udongo kwa kuondoa mabaki ya mimea kutoka juu ya udongo. Wakati wa kusaga mabaki hayo, huchanganya mabaki na punje za madini kwenye udongo na kutengeneza punje imara kwenye kinyesi chao, ambazo husaidia kuboresha muundo wa udongo. Kinyesi kinachotoka kwenye minyoo kinakuwa na naitrojeni mara 5 zaidi, fosfeti mara 7 zaidi, magadi mara 11 zaidi; na magnesia na kalsiam mara 2 zaidi kuliko udongo wa kawaida. Matobo yaliyotengenezwa na minyoo hukuza upenyezaji wa maji ya mvua na hewa kwa urahisi hivyo kuzuia mmomonyoko wa udongo na udongo kujaa maji. Minyoo ya ardhini inahitaji mabaki ya kutosha ya mimea, joto la wastani, fukuto na hewa ya kutosha. Ndio maana wanapenda sana hupunguza idadi ya minyoo kwenye udongo. Kutokana na shughuli zao nyingi na wingi wao, mchwa wanaweza kuchukuliwa kama wadudu wanaoleta manufaa kwa muundo wa udongo na sifa zake. Katika baadhi ya maeneo, hasa katika ukanda wa Sahel wa Afrika, mchwa kwa makusudi husambazwa shambani ili watafune mabaki ya miti kutengeneza mboji ambayo hutumika kama mbolea kwa kilimo. 
                Vijidudu muhimu zaidi ni bakteria, fangasi, mwani na protozoa. Bakteria kwenye udongo kama vile Rhizobium husaidia baadhi ya mimea kunyonya naitrojeni kutoka kwenye hewa. Fangasi kwenye udongo ndiyo hufanya sehemu kubwa ya vidudu vilivyopo. Mfano wa fangasi wa udongo ni spishi ya mycorrhizae. Mycorrhizae hustawi kwa mahusiano ya kutegemeana (mahusiano ambayo kila upande hunufaika) na takribani asilimia 90 ya mizizi yote ya mimea. Mizizi ya mimea hutoa sukari kwa ajili ya ukuaji wa fangasi. Na kinyume chake, fangasi wa mycorrhizae hutafuta kwenye udongo na kurudi na maji pia na virutubisho kama vile fosfeti, madini ya zinki na shaba ambavyo si rahisi kwa mimea kuvipata. Mycorrhizae pia huyeyusha madini kama vile fosifora, na kuzichukua hadi kwenye mmea, hufanya punje za udongo kuwa thabiti hivyo kuboresha muundo wa udongo, na kunyonya kaboni kutoka kwenye hewa na kuilimbikiza kwenye mboji ya udongo na punje za udongo zilizo thabiti. Kujumuishwa kwa viumbe hai kwenye udongo, kuendeleza kufunikwa kwa ardhi, kilimo mseto, na matumizi machache ya kemikali hupelekea kuongezeka kwa viumbe hai kwenye udongo. Katika mifumo ya kilimo hai na endelevu, uhai wa udongo ndio injini ya rutuba ya udongo na uzalishaji wa mazao, pia ndio mlezi wa afya ya udongo ya muda mrefu.

 Muundo wa udongo

 Muundo wa udongo unamaanisha mpangilio wa punje za udongo zinazounda matundu madogo na makubwa kati ya mabonge ya udongo. Muundo wa udongo ndio unaoshawishi jinsi maji yanavyopenya ndani ya udongo na kupitiliza, kiwango cha mzunguko wa hewa, uwezo wa udongo wa kuhimili mmomonyoko na jinsi mizizi ya mmea inavyokua kupitia tabaka za udongo. Matundu madogo ni mazuri katika kuhifadhi unyevu, wakati makubwa huruhusu upenyaji wa haraka wa maji ya mvua au umwagiliaji na kusaidia kuondoa maji kwenye udongo na hivyo kuhakikisha mzunguko wa hewa. Udongo hujikusanya pamoja na kugandishwa kwa njia mbalimbali. Katika baadhi za udongo ugandishaji wa punje huwa dhaifu sana, katika nyingine ni imara sana. Ukubwa wa mabonge katika baadhi ya udongo ni madogo madogo sana na laini, wakati katika aina nyingine mabonge ya udongo yana chembechembe na ni makubwa. Katika udongo wa aina nyingine, mabonge ni mazito na yana tundu chache, na katika nyingine mabonge yako wazi na yana matundu mengi. Katika udongo wenye muundo mzuri, chembechembe za madini na mboji ya kwenye udongo hutengeneza mabonge thabiti. Mchakato huu huchangiwa na viumbe hai kwenye udongo kama vile minyoo, bakteria na fangasi. Viumbe kwenye udongo hutoa taka mwilini ambazo hufanya kazi kama gundi na kugandisha chembechembe hizi pamoja. Fangasi zina aina ya nyuzi nyembamba zinazojulikana kama ‘haife’ ambazo hupenya kwenye udongo na kugandisha chembechembe za udongo pamoja. Mboji hufanya kazi kama aina ya gundi, kusaidia chembechembe za udongo kushikamana. Hii inaonyesha wazi kwamba muundo wa udongo unaweza kuboreshwa kwa kuongeza mboji na kukuza shughuli za kibiolojia za viumbe kwenye udongo. Wakati mbinu zisizo sahihi za udhibiti wa udongo kama vile kutifua ardhi wakati wa mvua husababisha mkandamizo, hii huweza kuharibika muundo wa udongo. Tabaka ngumu za udongo, udongo mgumu wa ufi nyanzi, ardhi kupasuka na mizizi kushindwa kupenya ni viashiria vya muundo wa udongo ulioharibiwa.


 Aina za udongo na sifa zake bainifu

 Kuna aina tofauti za udongo. Aina zote ni mchanganyiko wa aina tatu za chembechembe za madini: kichanga, mchangatope na mfi nyanzi. Kemikali zinazounda chanzo cha punje za udongo na jinsi punje hizi tatu zinavyounganishwa huamua aina ya udongo uliopo. Husaidia kujua sifa bainifu za msingi za udongo, iwapo udongo una asidi, alikali au hauna kitu chochote. Aina tofauti za udongo ni kama ifuatavyo: Udongo wa kichanga, udongo wa mchangatope, na udongo wa mfi nyanzi.

Udongo wa kichanga
 Udongo wa kichanga huundwa kutokana na kuvunjika vunjika na kumomonyoka kwa miamba kama vile mawe ya chokaa, matale, mawe meupe ya kung’aa na mwambatope. Udongo wa kichanga una punje kubwa ambazo zinaonekana kwa macho, na kwa kawaida zina rangi za kung’aa. Udongo wa kichanga huonekana kuwa na chenga ukiloweshwa au mkavu na hauminyiki unapouminya kwenye kiganja. Udongo wa kichanga hunyumbuka kwa urahisi na huruhusu unyevu kupenya kwa urahisi, lakini hauwezi kuuhodhi kwa muda mrefu. Huzoea haraka hali ya joto. Maji kupenya kwa urahisi huzuia matatizo ya kuoza mizizi. Udongo wa kichanga huruhusu maji kupitiliza zaidi ya kiasi kinachohitajika, ambayo husababisha mimea kukosa maji wakati wa kiangazi. Kwa hiyo iwapo mtu atapanda mimea katika udongo wa kichanga, itabidi kutegemea chanzo cha kudumu cha maji wakati wa kiangazi. Udongo wa kichanga una mboji kidogo sana na kwa kawaida una asili ya asidi. Kwa baadhi ya mazao kama peasi, ambayo huhitaji udongo wenye hali ya alikali ili uweze kutoa maua na kubeba matunda, kuna haja ya kuzimua hali ya asidi kwa kuongeza chokaa au kaboneti ya kalsiam kila mwaka ili kuendeleza hali inayofaa kwa kilimo. Udongo wa mchanga huathirika kwa urahisi na mmomonyoko hivyo inahitaji kukingwa dhidi ya upepo na mvua. Kupatikana kwa mboji mara kwa mara huboresha kwa kiwango kikubwa uwezo wake wa kuhifadhi maji na virutubisho, pia na uwezo wa kuzuia mmomonyoko. Matandazo pia husaidia udongo wa mchanga kuhodhi unyevu kupitia kupungua kwa mvukizo kutoka kwenye udongo


Mchangatope 

Mchangatope ni udongo wenye chenga ndogo zaidi kuliko udongo wa mchanga hivyo ni laini unapoushika. Udongo huu ukimwagiwa maji, unateleza kama sabuni. Unapoufi nyanga kati ya vidole vyako, unaacha uchafu kwenye ngozi. Mchangatope unapatikana katika maeneo asilia au kama tope katika tabaka kwenye maziwa, mito na bahari. Huundwa na madini kama vile mawe angavu ambayo yana madini aina ya kwatzi na punje ndogo ngodo za mabaki ya viumbe hai. Ni chengachenga kama udongo wa mchana lakini unahodhi virutubisho vingi zaidi na unyevu. Unatengeneza gamba kwa urahisi juu ya udongo, ambalo huzuia maji kupenya na unaweza kuzuia mimea isichomoze. Katika hali ya unyevu, hupenyeza maji kwa urahisi na ni rahisi zaidi kulima. Kadri mabaki ya viumbe hai yanavyokuwa mengi, ndivyo inavyonyonya maji ya mvua vizuri zaidi na kuendeleza muundo wake hata baada ya mvua kubwa, hivyo kuzuia mmomonyoko. 

Udongo mfinyanzi

 Udongo mfinyanzi huundwa na chembe chembe ndogo sana ambazo zina sehemu ndogo sana ya kupitisha hewa. Udongo mfi nyanzi huundwa baada ya miaka mingi ya miamba kumomonyoka na athari za hali ya hali ya hewa. Pia hutengenezwa kama mashapo yaliyotua baada ya mwamba kupasuliwa vipande vipande na hali ya hewa, kumomonyolewa na kusafi rishwa. Udongo mfi nyanzi kutokana na mchakato wa uundwaji wake unakuwa na madini mengi sana. Udongo mfi nyanzi unateleza na kunata unapokuwa mbichi lakini laini unapokauka. Udongo mfi nyanzi huhodhi unyevu vizuri, lakini haupenyezi maji vizuri, hasa unapokuwa mkavu. Mara nyingi vidimbwi hutokea kwenye udongo mfi nyanzi na udongo hugandamizwa kwa urahisi. Kutokana na uwezo wake mdogo wa kupenyeza maji, hatari ya maji kutuama na ardhi kuwa ngumu, sio rahisi kufanya kazi na udongo mfi nyanzi. Kuongeza mboji na jasi huboresha hali ya udongo na kuufanya kulimika kwa urahisi. Jasi na mboji hutenganisha chembe chembe za udongo mvinyanzi na hivyo kuruhusu maji kupenya na kuhodhiwa kwa usahihi. Kuongeza mabaki ya viumbe hai kwenye udongo hukuza kuongezeka kwa minyoo ya ardhini, ambayo husaidia kuinua ubora wa udongo. 

Udongo tifutifu 

Udongo tifutifu hutengenezwa na uwiano mzuri wa mchanga, mchangatope, mfi nyanzi na mabaki ya viumbe hai. Huchukuliwa kama udongo unaofaa zaidi katika ardhi inayolimika. Udongo tifutifu una rangi nyeusi na unafanana na kushika unga mikononi. Umbile lake ni mchanga mchanga na huhodhi maji kirahisi sana, hata hivyo upenyezaji wake wa maji ni mzuri. Kuna aina nyingi za udongo tifutifu kuanzia wenye rutuba hadi ulio na tope zito na tabaka nene la juu. Hata hivyo kati ya aina zote hizi tofauti za udongo, udongo tifutifu ndio unaofaa zaidi kwa kilimo.

awali kabsa kwenye makala ya Njia ya kutambua aina ya udongo shambani kwako nilieleza juu ya kufanya upembuzi wa udongo kama utakuwa umekosa mtaalamu au unaweza kufanya mwenyewe na kumpa mtaalamu majibu ili akupe ufafanuzi juu ya majibu uliyopata
pia katika makala ya Njia za kuondoa magadi(salt) shambani nilieleza juu ya namna magadi yanavyoharibu mazao na kurudisha nyuma uzalishaji kwani wakulima wanawekeza sana kwenye inputs nyingine na kusahau kitu cha muhimu ambacho ni udongo 

Kwa ajili ya kupima udongo na kupata ushauri juu ya kilimo basi wasiliana na mimi mwenyewe kwa number za simu au email hapo chini 
sehemu ya pili nitaeleza kuhusu rutuba ya udongo,tabia za udongo wenye rutuba,kiasi stahiki cha virutubishwo vya mmea na mambo mengine mengi kuhusu udongo ili kukusaidia wewe mkulima uweze kuongeza uzalishaji na ukuze kipato chako

pia ukitaka makala hizi kwa mfumo wa pdf wasiliana na mimi pia

Octavian Jutine Lasway 
Irrigation and Water resources Engineer 
Green Agriculture
0763347985
octavianlaswai@gmail.com
Reactions:

3 comments:

Unknown said...

Nc it help me thanx

Unknown said...

Yaaani objectives tu zmenifanya nitake kujua nn zaidi kipo mdani ya somo la leo
Ahsante Eng

Anonymous said...

good article

YouTube

GREEN HOUSE

GREEN HOUSE
BEST DESIGN

Visitors

LIKE US ON FACEBOOK

AGRICULTURE LAND

Mostly Visited