Habari ndugu msomaji wa wetu wa makala za kilimo, Natumaini
tunaendelea vizuri na mapambano ya kila siku. Leo tutaanza kujifunza kilimo cha
bora cha nyanya, na tutaanza kufahamu vitu vya msingi kwanza, na natumaini
ukimaliza mfululizo wa makala hizi utakua mkulima hodari wa nyanya. Kila kitu
lazima kiwe na msingi imara, karibu tujifunze wote:
Utangulizi:
• Nyanya ni zao la mboga ambalo hulimwa sehemu nyingi
duniani kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na pia kama zao la biashara.
Inahisiwa kuwa asili ya nyanya ni nchi ya Peru/Equador huko Amerika ya Kusini.
Mmea huu ulianza kuzalishwa kama zao katika nchi ya Mexico na baadaye kusambaa
katika nchi nyingine za ulimwengu.
Uzalishaji wa nyanya duniani na hapa Tanzania
Nchi zinazolima nyanya kwa wingi duniani ni pamoja na USA,
Italia na Mexico. Kwa upande wa Africa nchi zinazo lima ni kama; Malawi, Zambia
na Botswana.
Zao hili hulimwa pia katika nchi za Africa Mashariki,
ikiwemo Kenya, uganda,Tanzania, Rwanda na Burundi
Zao la nyanya linalimwa karibu maeneo yote ya Tanzania.
Uzalishaji wa nyanya ni mkubwa kuliko mazao mengine ya mbogamboga yanayolimwa
hapa Tanzania, uzalishaji wa nyanya kwa mwaka ni jumla ya tani 129,578
ikiwakilisha asalimia 51 ya mazao yote ya mboga. Kwa mujibu wa Wizara ya kilimo
ya Tanzania maeneo yanalolima sana nyanya ni pamoja na Mkoa wa Kilimanjaro
(Hai, Moshi na Rombo), Arusha (Arumeru), Morogoro (Mgeta), Tanga (Lushoto),
Mbeya (Mbeya vijijini) na Singida. Morogoro ndiyo inayoongoza kwa kilimo hichi
ikiwa na wazalishaji wenye zaidi ya hekta 6,159 (ekari 15,398). Pamoja na
kwamba eneo la uzalishaji linaongezeka kwenye maeneo mengi lakini uzalishaji wa
nyanya bado ni mdogo sana.
Uzalishaji mdogo unasababishwa na kupungua kwa rutuba ya
ardhi, upepo, joto, ukame. Sababu nyingine ni pamoja na ukosefu wa aina za
nyanya zenye mavuno mengi amabazo zinahimili mazingira ya kwetu, wadudu,
magonjwa na magugu.
Mazingira
• Hali ya Hewa:
Nyanya hustawi vizuri zaidi kwenye mazingira ya joto la
wastani kuanzia nyuzi joto 18-27 sentigreti. Mvua nyingi husababisha mlipuko wa
magonjwa ya ukungu kama vile Baka jani chelewa n.k.)
• Udongo:
Nyanya hustawi kwenye aina zote za udongo kuanzia udongo wa
kichanga, mweupe wa tifutifu hadi udongo wa mfinyanzi, ili mradi uwe na mboji
ya kutosha na usiosimamisha/tuamisha maji. Pia uwe na uchachu wa wastani yaani
pH 6.0 - 7.0.
Aina za Nyanya
Kutokana na tabia ya ukuaji, nyanya zinagawanyika katika
makundi mawili:
1. Aina ndefu ( intermediate) kwa mfano ANNA F1, Tebgeru 97.
Aina hizi hufanya vizuri zaidi zinapopandwa ndani ya greenhouse. Uvunaji wake
ni wa muda mrefu, zipo ambazo zinavunwa hata zaidi ya miezi 6, yaani hiyo miezi
6 ni ya uvunaji.
2. Aina fupi (determinate) kwa mfano Tanya, Cal J, Mwanga,
Onyx, Roma VF (nyanya mshumaa)
Kotokana na uchavushaji, nyanya zinagawanyika makundi
mawaili:
1. OPV (Open Pollinated Variety) - Aina za kawaida
2. Hybrid – Chotara: Hizi ni aina zenye mavuno mengi, kati
ya hizo zipo aina fupi na ndefu.
Katika karne hii ya 21, nyanya zinazopendelewa kulimwa zaidi
na wakulima, ni zile zinazoweza kuvumilia magonjwa, zinazo zaa sana, na zenye
ganda gumu ili kufanikisha usafirishaji, na kuhifadhika kwa siku nyingi bila
kuharibika mapema.
Kuandaa Kitalu cha Nyanya
Mambo muhimu ya kuzingatia:
• Kitalu kiwe karibu na maji ya kutosha na ya kudumu
• Kiwe sehemu iliyowazi na yenye udongo ulio na rutuba ya
kutosha
• Eneo la kitalu kama ni kubwa liwe tambarare au na mwiinuko
kidogo ili kuepuka maji yasituame kwenye kitalu, mtelemko ukiwa mkali sana nao
sio mzuri kwani husababisha mmomonyoko wa udongo.
• Kitalu kiwe sehemu ambayo haikuwa na zao la nyanya au
viazi mviringo (au mazao ya jamii ya nyanya k.m. mnavu, biringanya n.k.)
• Kiwe sehemu ambayo ni rahisi kupata huduma zote muhimu kwa
urahisi, ikiwa ni pamoja na uhamishaji wa miche kwenda sehemu nyingine. Pia
kurahisisha usambazaji wa miche kwenda sehemu nyingine.
Kuandaa Matuta ya Kusia Mbegu za Nyanya
Aina ya matuta:
– matuta ya makingo (sunken seed bed)
– matuta ya kunyanyulia udongo (raised seed bed)
– matuta ya kawaida (flat seed beds)
Mambo Muhimu ya Kuzingatia wakati wa Kuandaa Matuta
• Tuta liwe na upana kati ya sentimita 90-120, na urefu
wowote, [ili mradi muhudumu anaweza kutoa huduma nyingine zote kitaluni bila
kukanyaga miche].
• Kwatua/lima kina kirefu cha kutosha kiasi cha sentimita
15-20 ili mizizi iweze kusambaa vizuri ardhini.
• Choma takataka juu ya kitalu, au funika tuta kwa nailoni,
majuma 4-8 ili kuua vimelea vya magonjwa na wadudu.
• Wakati wa kuandaa, kitalu, ongeza mbolea aina ya samadi/vunde
au mboji kwenye udongo kisha kwatua ili ichanganyike vizuri na udongo.
• Changanya kiasi cha debe 1 hadi 2 kila baada ya mita moja
(hatua moja) mraba.
• Tuta lisiwe na mabonde mabonde au mawe mawe ambayo
yanaweza kuzuia usambaaji mzuri wa mbegu kwenye tuta, lisawazishwe vizuri ili
kuhakikisha usambazaji mzuri wa mbegu na kuepuka mbegu kufukiwa chini mno kiasi
ambacho hazitaota.
Faida na Hasara za Matuta yaliyotajwa hapo juu
1. Matuta ya kunyanyulia udongo (raised seed beds);
– matuta ya namna hii huruhusu maji, hewa na mizizi kupenya
kwenye udongo kwa urahisi zaidi.
– Mazao ya mizizi hupata nafasi ya kutosha kutanuka haraka
zaidi
– Matuta haya hayatuamishi maji kama mengine, hivyo hutumika
zaidi kwenye maeneo yanayokuwa na mvua mara kwa mara.
Hasara:
o Matuta ya namna hii yana sababisha sana mmomonyoko wa
udongo kama hayakutengenezwa vizuri.
2. Matuta ya makingo (sunken seed beds):
Faida:
· matuta haya ni rahisi kutengeneza
· hutumika wakati wa kiangazi ili kuhifadhi maji na unyevu
· nyevu mdogo unaopatikana ardhini
· ni rahisi kumwagilia kwa kutumia maji ya mfereji au bomba
· huhifadhi unyevu nyevu kwenye ardhi kwa muda mrefu
· huzuia mmomonyoka wa ardhi
Hasara:
· Matuta ya aina hii hayawezi kutumika kwenye maeneo yenye
· mvua nyingi.
3. Matuta ya kawaida (flat seed beds):
Faida:
· ni rahisi sana kutengeneza kwani udongo ukisha kwatuliwa
· na kusambazwa mbegu huoteshwa
· ni rahisi kutumia eneo kubwa kuotesha mbegu
Hasara:
Matuta ya aina hii hayawezi kutumika kwenye maeneo yenye
mvua nyingi.
Kusia Mbegu
• Hakikisha ubora na uotaji wa mbegu kabla ya kuzipanda
kitaluni (germination test)
• Weka mistari kwenye tuta kulingana na ukubwa wa tuta,
lakini mistari isiwe chini au zaidi ya sentimita 15-20 toka mstari hadi mstari
•Kina cha mistari kisiwe cha kutisha bali kiwe kati ya
sentimita 1-2
• Matuta yapate maji ya kutosha siku moja kabla ya kusia
mbegu. Ni vizuri kutumia chombo cha kumwagilia (watering can).
• Mbegu ziatikwe kwenye mistari na zisambazwe vizuri ili
kufanikisha usambaaji mzuri wa mbegu kwenye tuta. Changanya mchanga laini na
mbegu kisha sambaza kwenye mistari iliyoandaliwa kwenye tuta.
Mbegu zinaweza pia kuatikwa kwenye tuta bila mistari, lakini
zisambazwe kwa uwiano mzuri kwenye tuta ili kupunguza msongamano. Msongamano
husabisha magonjwa ya fangasi kama vile kinyausi (damping off) au ukungu
(blight).
• Weka matandazo kiasi cha kutosha ambacho hakitazuia kuota
kwa mbegu.
• Mara baada ya kuatika mbegu, mwagilia maji kiasi cha
kutosha kulingana na unyevu nyevu ulioko ardhini
Mambo ya Kuzingatia baada ya kusia mbegu pamoja na Matunzo
Kitaluni
• Mwagilia maji kwenye kitalu baada ya kuotesha kulingana na
unyevu nyevu uliopo kwenye udongo.
• Miche yote ikisha ota, ondoa matandazo, kisha weka chanja
ili kupunguza mionzi ya jua ambayo inaweza kuunguza miche michanga. (kipindi
cha baridi si muhimu sana)
• Punguzia miche (thinning) ili ibakie kwenye nafasi ya
kutosha. Hivyo miche ibakie kwenye umbali wa sentimita 2.5 - 4. Hii itapunguza
magonjwa ya ulemavu na mnyauko, pia itasaidia kupata miche bora na yenye nguvu.
• Endelea kumwagilia hadi miche ifikie kimo kinachofaa
kuhamishia shambani.
• Punguza kiwango cha umwagiliaji maji, siku chache kabla ya
kuhamishia miche shambani, yaani siku 7-10.
Kanuni na Mbinu za kuhamisha miche toka Kitaluni kwenda shambani (Transplanting Rules)
• Mwagilia miche masaa machache kabla ya kuhamishia miche
shambani ili wakati wa kung’oa miche mizizi ishikamane vizuri na udongo.
• Kabla ya kuhamisha miche, mashimo yawe yamekwisha andaliwa
katika nafasi zinazo stahili huko shambani.
• Miche ihamishwe wakati wa jioni ili kuepuka madhara
yanayoweza kusababishwa na jua.
• Kwa ujumla karibu mazao yote ya mboga mboga huwa tayari
kuhamishiwa shambani yakiwa na majani kamili kati ya 2-6 pamoja na mizizi mingi
iliyostawi vizuri.
• Mche lazima uwe na afya nzuri, uwe umenyooka vizuri, hivyo
miche yote iliyonyongea au myembamba kupita kiasi isichukuliwe wakati wa
kupeleka shambani.
• Ng’oa miche kwa uangalifu hasa pamoja na udongo wake kwa
kutumia vifaa husika ili mizizi isidhurike.
• Miche ihamishiwe shambani mapema mara baada ya kung’olewa
toka kitaluni.
• Wakati wa kuhamisha miche, uangalifu mkubwa utumike ili
kutoharibu miche/mizizi.
Maandalizi ya Shamba la Nyanya
• Shamba la nyanya liandaliwe mwezi 1-2 kabla ya kupanda
miche.
• Mara baada ya kulima choma nyasi juu ya udongo au ondoa
magugu yote yanayoweza kuhifadhi wadudu na magonjwa ya nyanya.
• Siku moja au mbili kabla ya kuhamishia nyanya shambani,
mwagilia sehemu iliyoandaliwa kwa ajili ya kuhamishia nyanya.
• Nafasi kati ya mche hadi mche ni wastani wa sentimita
(50-60) x (50-75) kutegemeana na aina au hali ya hewa. Kama ni kipindi cha
baridi ni vyema nyanya zikapandwa mbalimbali ili kuruhusu mzungungo wa hewa na
kuzuia magonjwa ya fangasi.
Jinsi ya kupanda miche:
• Hamisha miche toka kitaluni pamoja na udongo wake
• Sambaza mizizi vizuri kwenye shimo bila kukunja.
• Fukia miche kina kile kile ambacho shina lilikuwa
limefukiwa bustanini.
• Mwagilia maji ya kutosha kulingana na unyevunyevu uliopo
kwenye udongo kasha weka matandazo na kivuli ili kupunguza uharibifu
unaosababishwa na mionzi ya jua.
Mambo muhimu ya kuzingatia baada ya kuhamishia Miche
Shambani
• Kagua shamba mara kwa mara ili kujua maendeleo au matatizo
yaliyoko shambani mapema
• Hakikisha shamba ni safi wakati wote, palilia shamba na
hakikisha magugu yote hasa yale ya jamii ya nyanya yamelimiwa chini.
• Ondoa mimea iliyoshambuliwa na magonjwa au ondoa sehemu
zilizoshambuliwa, kisha zifukiwe chini au kuunguza moto.
• Punguza matawi na vikonyo ili kuongeza mwanga wa kutosha
kwenye nyanya pamoja na kuruhusu mzunguko wa kutosha wa upepo na kusababisha
mazingira magumu ya wadudu maadui kwenye nyanya, hasa wale wanaopenda kiza na
magonjwa yanayopendelea unyevunyevu.
soma zaidi kuhusu kilimo cha Tikiti maji,vitunguu,Tangawizi
Octavian Justine Lasway soma zaidi kuhusu kilimo cha Tikiti maji,vitunguu,Tangawizi
Irrigation and water resources Engineer
1 comments:
Asante Sana kwa makala hii,naendelea kuwa na wewe kwenye website hii.
Ubarikiwe na upate maisha malefu.
Post a comment