Tuesday, 6 March 2018

 MWONGOZOWA KILIMO BORA CHA MAHINDI 

Agronomist Allen Lupembe
+255717316354 

                     
UTANGULIZI
Mahindi ni zao muhimu la chakula, na ni aina ya nafaka inayotumiwa zaidi kama chakula,uhususani katika matifa ya Afrika, na yamekuwa yakitumika zaidi na nchi zilizopo kusini mwa jangwa la Sahara. Ni chakula cha matumizi ya nyumbani kwa idadi ya watu inayokadiriwa kuwa asilimia 50. Ni chanzo muhimu cha madini na kuongeza nguvu mwilini, protini, madini ya chuma (iron) vitamini na madini mengine asilia.Waafrika
hutumia mahindi kwa njia mbalimbali (uji, ugali na pombe). Na mahindi ya kuchoma.
Kila sehemu ya mmea wa mahindi ina thamani kiuchumi : punje, majani, shina na magunzi   huweza kutoa kiasi kikubwa cha bidhaa nyinginezo zilizo chakula na zisizokuwa chakula.
Vile vile mahindi ni chakula muhimu cha mifugo (ng’ombe) na huhifadhiwa kama silage. Pia mabaki ya mimea na nafaka hutumika viwandani kutengeneza wanga na mafuta.
Mahindi ni mimea ambayo hustahimili mabadiliko ya hali ya hewa tofauti tofauti na huweza kumea katika maeneo mengi tofauti hapa nnchini. Kuna aina nyingi za mahindi yanayotofautiana katika muda wa kukomaa, mavuno na ustahimilivu wa hali ya hewa.

HALI YA HEWA NA UDONGO
Mmea huu unahitaji kiwango cha joto cha kila siku cha nyuzi joto 20º ili umee vyema. Joto la juu sana kwa mazao mazuri ni kama nyuzi joto 30º. 
Mahindi hustawi katika maeneo mbalimbali hapa nchini kuanzia 0-3000 m kutoka usawa wa bahari kulingana na aina ya mbegu na hali ya hewa ya eneo husika. 
Mahindi huwa yanaathirika sana na ukosefu wa unyevu wakati wa kutoa maua na matunda. Pia yanahitaji maji ya kutosha wakati wa kupanda. Katika nchi za joto jingi (tropiki), mahindi hufanya vyema katika mvua ya kiwango cha milimita 600 hadi 900 wakati wa kukua.
Mahindi yanaweza kukuzwa kwenye aina nyingi za udongo lakini hukua vyema zaidi katika udongo wa kichanga au tifutifu usiotuamisha maji mengi, ulio na hewa ya kutosha na ulio na rutuba na madini ya kutosha. Pia hustawi vizuri katika udongo wenye uchachu wa kiwango cha pH 6-6.5.
Pia ikumbukwe kuwa mahindi ni moja ya zao ambalo huathirika sana na hali ya chumvi katika maji na udongo. 

KUTAYARISHA SHAMBA

SHAMBA LILILO ANDALIWA VIZURI

Shamba la mahindi linahitajika kutayarishwa mapema  mapema sana mwanzoni mwa msimu wa mvua au hata kabla mvua kuanza.

Shamba linaweza kuandaliwa kwa aina tofauti tofauti kulinganisha na eneo na aina ya udongo. Shamba linaweza kulimwa kwa trekta au kwa jembe la mkono kwa kina kisichopungua 15 cm ili kuruhusu mizizi kupenya vizuri na udongo kuhifadhi maji kwa wingi. Kama shamba liaasili ya kutuamisha maji matuta yaandaliwe vizuri shambani. Moto usitumike wakati wa kuandaa shamba.
          Vilevile kama shamba lina asili ya mmomonyoko wa udongo, basi ni vyema tahathari ichukuliwe katika uhifadhi wa udongo na unyevunyevu ardhini kwa kuweka matandazo shambani (mulching).

FAIDA ZA KUANDAA SHAMBA MAPEMA

Baada ya kuvuna,udongo bado ni mlaini hivyo hulimika kwa urahisi kwa kutumia jembe lolote.
 Masalia yatakayofunikwa udongoni huoza mapema.
 Hupunguza magugu.
 Hupunguza wadudu waharibifu na kuharibu mazalio yao.
 Mahindi yanapata mvua ya kutosha hadi kukomaa.
 Magonjwa kama yale ya ya majani (streak ugonjwa wa milia) hayatatokea au
yatakuwa kidogo.
 Mbolea uliyoweka itayeyuka pamoja na mahindi na yatastawi vizuri.

WAKATI WA KUPANDA

Wakati wa kupanda hutatanisha kwani mvua haitabiriki,Kama mvua hunyesha nyakati na majira yale yale ya mwaka basi kalenda ifuatayo inaonyesha tahere za kupanda zao la mahindi katika eneo lako.
 Mbeya na maeneo ya jirani, mwanzoni mwa mwezi Novemba hadi Desemba
mwishoni.
 Morogoro,Pwani, DSM, Tanga na Maeneo Jirani Mwezi Januari, February na March Mwanzoni katikati
 Iringa na maeneo ya jirani, katikati ya mwezi Novemba hadi Desemba mwishoni
 Songea na maeneo ya jirani, katikati ya mwezi Novemba hadi Januari mwanzoni.
Kupanda mahindi mapema ni muhimu kwani uwezekano wa kuvuna mazao mengi ni
mkubwa. Kwa mashamba makubwa sana wakati wa kupanda uwe wiki moja kabla ya mvua
kuanza kunyesha na isizidi wiki mbili kabla ya mvua. Isiwe mapema zaidi kwani mbegu
zitaharibiwa na joto katika na wadudu, panya, ndege na wanyama wengineo.

KUCHAGUA MBEGU BORA

Mbegu bora ni zile zilizo zalishwa kitaalamu.
 Ni safi hazijabunguliwa na wadudu.
 Huzaa mazao mengi.
 Hustahimili magonjwa.

AINA ZA MBEGU Mbegu aina ya chotara(hybrid)
 Aina ya ndugu moja(synthetic)
 Mbegu aina ya composite
Mbegu za kisasa zikitumiwa vizuri katika misingi ya kilimo zina uwezo wa kuzaa magunia
50-80 au tani 5.5 – 7.5 kwa hekta moja.8( Gunia 25

MAPENDEKEZO YA MBEGUZA KUPANDA

Kuna mbegu nyingi za kisasa zilizoko kwenye soko mfano wa ZAMSEED, SEEDCO ,PANNAR, MERU n.k


KUPANDA

Idadi ya mimea katika eneo ni muhimu kwani ikizidi
 Kuna uwezekano wa mazao kupungua.
 Mimea kuwa dhoofu
 Mimea mingi kutozaa au kuwa na matunda madogomadogo.
 Kunakuwa na uwezekano mkubwa wa kusambaa kwa magonjwa kiurahisi
Idadi ya mimea nayo ikipungua kwenya eneo husababishwa mavuno kupungua
jambo la kufanya ni kupanda mbegu katika nafasi na kiwango cha mbegu sahihi kilichoshauriwa na mtaalamu hapo chini.

KIASI CHA KUPANDA
 Kiasi cha kilo 20(ishirini) za mbegu kinatosha kupanda hekari moja., (Hii hutegemea na aina ya mbegu)

NAFASI ZA KUPANDA.

MASHINE YA KUPANDIA

Unaweza kupanda mhindi katika nafasi mbalimbali kulingana na mahitji yako, hali ya hewa na rutuba ya udongo. lakini zifuatazo ni nafasi pendekezwa na hutumika sehemu nyingi hapa nchini kwetu.
 75cm x 30cm mfano:- mstari kwa mstari 75cm na mche kwa mche 30cm hii ni kwa mbegu moja kwa kila shina na kufanya uwe na idadi ya mimea zaidi ya 44000 kwa hekta.
 75cm x 60cm mfano;- mstari kwa mstari 75cm na mche kwa mche 60cm hii ni kwa mbegu mbili  kwa kila shina na kufanya uwe na idadi ya mimea 44000 na zaidi kwa hekta.
 75cm x 25cm mfano:- mstari kwa mstari 75cm na mche kwa mche 25cm hii ni kwa mbegu moja kwa kila shina na kufanya uwe na idadi ya mimea zaidi ya 53000 kwa hekta. 
 90cm x 50cm Hii ni nzuri kwa sehemu kame na kwa wanaopanda mazao  mchanganyiko au kilimo mseto.
Mahindi yanaweza kuchanganywa na  mazao mengine ya kutambaa kama kunde, maharage, maboga, karanga nk.
Image result for good maize spacing
Shamba la mahindi lililopandwa kwa nafasi sahihi na kiasi cha mbegu sahihi.


MATUMIZI YA MBOLEA

 Mahindi hustawi na kuzaa vizuri iwapo yatapatiwa mbolea pamoja na matunzo mengine ya kilimo bora.
 Angalizo: Ukipanda mbegu bora bila kutumia mbolea ni kazi bure.

KUNA AINA MBILI KUU ZA MBOLEA

 Mbolea za asili mfano; samadi,mboji na majani mabichi,mbolea hizi hua na
virutubisho vya kutosha ambavyo havijulikani vipo kwa kipimo kiasi gani.
 Mbolea za viwandani, hizi hua na virutubisho vya kutosha na vipimo hujulikana, hii
inasaidia kujua ni kiasi gani kitumike kwa kipindi gani.

KWA MFANO:
Mbolea inayotumiwa na wakulima wadogo mara yingi huwa haitoshi. Mahindi ya kiwango cha juu yaweza tu kufikia kiwango cha juu cha Uzalishaji iwapo yatapewa lishe na madini ya kutosha. Mahindi ya tani 2 kwa hekta na tani 5 kwa hekta hutumia karibu kilo 60 N, kilo 10 za P205 na kilo 70 K20 kutoka katika udongo. Mahindi hunyonya Nitrogen pole pole katika miezi ya kwanza baada ya kupanda, lakini huongezeka hadi kiwango cha juu kabisa
wakati wa kutoa maua na kukuza tunda (gunzi). Mahindi huhitaji nitrogen kwa kiwango cha juu na ukosefu huwa ndio kizingiti. Kiwango cha juu cha nitrogen kinahitajika mara tatu; kwanza wakati wa kupanda, pili, wakati ambapo mmea umefikia sentimita 50 za urefu na tatu, wakati matunda ya mahindi yanaanza kutoa zile nyuzi nyuzi nyororo (silking). Udongo mwingi huwa na madini ya phosphorous (P205) na potassium (K20) lakini siokiwango kinachotosheleza mahitaji haswa ya mbegu za mahindi zinapochipua. Nyunyuzia P205 karibu na mbegu ili ziote kwa haraka. K20 hutumika kwa kiwango kikubwa lakini hitaji la mimea hubainika baada ya upimaji wa hali ya udongo kujua kiasi cha mahitaji (soiltest). (ndo maana twasisitiza mbolea za viwandani sio lazima iwe ya kemikali).


DALILI ZA UPUNGUFU WA MBOLEA

Ukosefu wa K20 husababisha ncha za majani kuwa na rangi ya njano na kuunda gunzi (cob)
lisilo na punje hadi juu. Ukosefu wa P205 hufanya matawi kuwa na rangi ya samawati na mbegu zisizo laini. Dalili za ukosefu wa nitrogen ni majani ya rangi ya manjano na mimea dhaifu mifupi. Phosphate haifyonzwi haraka na mahindi na pia udongo mwingi wa nchi za joto hukosa madini hayo ya phosphate. Inashauriwa unyunyuzie mbolea ya kiasili kama samadi kabla ya kulima ili uboreshe hali ya udongo na kuongezea madini. Katika ukulima wa kiasili, (organic farming), Nitrogen (N) hutiwa kwenye udongo kupitia kwa upandaji wa mimea ya jamii ya mikunde (legumes) ambayo hutoa nitrogen katika hewa, Hata hivyo mapendekezo ya kimbolea yaliyo katika misingi ya uchunguzi wa udongo hutoa nafasi nzuri ya kupata kiasi kizuri cha mbolea bila kuweka kiwango cha chini au juu.
Omba msaada kutoka kwa mafisa ugani wa kilimo walio katika eneo lako. Katika maeneo yanayo tegemea mvua kukuza mahindi, panda mbegu wakati wa mvua ya kwanza. Hii
itaruhusu mizizi kunyonya madini yaliyotengenzwa na bakteria katika udongo. Maji yaliyosimama huyeyusha na kuondoa madini ya nitrogen kutoka katika udongo na kusababisha ukosefu wa Nitrogen.
Image result for maize nutrient deficiency
Upungufu wa madini ya Phosphorus P
Image result for maize nutrient deficiency
Upungufu wa madini ya Pottasium K


Image result for maize nutrient deficiency
Upungufu ya madini ya Nitrojeni N
KUDHIBITI MAGUGU
SHAMBA LILILPO FANYIWA PALIZI KWA KUTUMIA DAWA

Udhibiti wa magugu ni muhimu sana. Katika wiki 4 hadi 6 za mbele baada ya kumea, mahindi huathiriwa sana na magugu. Ni lazima mahindi yapandwe mara moja baada ya kutayarisha shamba. Na usiache magugu mpaka yawe makubwa ndipo uanze kupalilia.
Unaweza kulima katikati ya laini za mahindi ili udhibiti magugu.
Nchini Tanzania, kupalilia mara mbili kunahitajika kwa aina nyingi za mahindi, ingawa kupalilia kwa mara ya tatu kutahitajika kwa aina ambazo zinahitaji zaidi ya miezi 5. kukomaa. Njia rahisi za kupalilia kunaweza kufanywa kwa mkono au kwa jembe la mkono ama kwa kutumia viuagugu ambavyo vimethibitishwa. (Angalizo; usitumie viuagugu bila ushauri wa kitaalam)

UHUSIANO WA NIPE NIKUPE

Desmodium (desmodium uncinatum) nyasi ya Molasses (melinis minutifolia) zikipandwa kati kati ya laini za mahindi huzuia wadudu kama stalk borers moths. Mimea hii hutoa kemikali ambazo huwafukuza wadudu aina stem borers’ moths. Zaidi ya hayo Desmodium huzuia gugu haribifu,witchweed striga hermonthica. Napier grass (pennisetum purpureum) na Sudan grass (sorghum vulgare sodanese) ni mimea mizuri sana inayonasa wadudu aina ya stem borers. Napier grass ina njia yake madhubuti ya kujikinga dhidi ya wadudu wanaotoboa mmea kwa
kutoa utomvu kutoka kwenye shina, ambayo huzuia wadudu kufyoza mmea na kusababisha uharibifu. Nyasi hizi pia huvutia adui wa stem borers kama mchwa, earwigs na
buibui. Nyasi aina ya Sudan pia husaidia maadui asilia, kama nyigu (parasitic wasp).
Mahindi huweka kivuli kwenye mimea ya mboga mboga ikipandwa safu moja katikati ya mboga kwenye maeneo yaliyo na jua kali. Hii huongeza mazao ya mboga zilizopandwa hivi, na mimea jamii ya mikunde huongeza nitrogen kwenye udongo ambayo huitajika zaidi katika ukuaji wa mahindi pia hupunguza wadudu aina ya (leafhoppers, leafbeatles, stalk borers na fall army worm), upandaji wa mimea jamii ya mikunde ufanyike mara baada ya palizi ya kwanza.

UVUNAJI NA UHIFADHI

Mahindi huvunwa mara baada ya kukomaa, yanaweza kuvunwa kwa mikono au kwa kutumia mashine maalum ya kuvunia kama shamba ni kubwa. Mahindi yaliyokomaa vizuri huwa na majani ya njano na punje ngumu zilizoshiba. Ili mahindi yawe tayari kuvunwa, huachwa shambani mpaka yakauke vizuri kabisa na majani yote kukauka na kabisa na hali ya unyevunyevu wa punje kufikia asilimia 15-20%. Mahindi yakiachwa sana shambani huaribiwa na wadudu kama mchwa na dumuzi, pia kama mahindi yakivunwa yakiwa bado hayajakauka vizuri au kukomaa vizuri ni rahisi sana kubunguliwa. Hivyo ni vyema kuzingatia muda mzuri wa kuvuna. Pia uvunaji wa mahindi kipindi cha mvua nyingi hupelekea mahindi kuharibika kama yatahifadhiwa yakiwa yameloweshwa na mvua.
Kuna changamoto nyingi sana hutokea kipindi cha uhifadhi mahindi zikiwemo ukaushaji wa mahindi katika kiwango kinachohitajika (13% grain moisture content), kuzuia wadudu na wanyama waharibifu. Mahindi yakihifadhiwa katika hali ya unyevunyevu na joto kali hupelekea mahindi kuota ukungu ambao huzalisha sumu iitwayo aflatoxin na kufanya mahindi hayo yasifae kabisa kwa chakula cha binadamu. 
Ili kuhifadhi mahindi vizuri, kausha mahindi yako katika jua kali mpaka kiwango cha unyevunyevu katika punje kufikia 13%. Njia rahisi ya kujua mahindi yapo katika hali ya 13% ni hivi, baada ya kukausha mahind yako juani chukua punje kadhaa jaribu kuuma punje moja moja. Ukiona punje ni laini na inapasuka kirahisi baada ya kuuma basi endelea kuaniaka mahindi yako tena mpaka yawe magumu kabisa. Baada ya hapo unaweza ukachanganya dawa za kuulia wadudu katika mahindi yako na kuyajaza katika viroba/mifuko na kuhifadhi gharani. Pia unaweza kuhifadhi mahindi yako katika chombo ambacho hakipitish hewa kama pipa, jaba n.k. Vilevile kuna njia mbadala ya kuhifadhi mahindi katika njia mbadala ya mifuko maalumu ambayo huitaji kuweka sumu ya aina yoyote. Baada ya hapo panga magunia yako gharani vizuri. hakikisha ghara ni safi, kavu na hakuna upenyo wa kuruhusu wadudu na wanyama waharibifu kuingia.

WADUDU NA MAGONJWA YA MAHINDI

WADUDU

Wapo wadudu wengi sana ambao hushambulia mahindi yakiwa shambania na yakiwa yamehifadhiwa gharani, hivyo ni vyema mkulima kuwatambua wadududu wasumbufu shambani na jinsi ya kukabiliana nao. 

1. Viwavijeshi /African Amyworm (Spodoptera exempta)
Wadudu hawa ni hatari sana katika mazao ya nafaka na hutokea kwa mlipuko. Wanauwezo wa kuangamiza shamba kubwa kwa muda mfupi sana na kuhamia shamba lililo karibu.
Wadudu hawa unaweza kukabiliana nao kwa kufanya ukaguzi mara kwa mara wa shamba lako na mara tu uonapo dalili za kuwepo unaweza kuwaangamiza kwa sumu ambayo inaweza kuwaangamiza kirahisi kabla ya kuleta tatizo kubwa. Pia ni vyema kuandaa shamba mapema na kuweka shamba katika hali ya usafi ili kuzuia mazalia na kuondosha mabaki yao.

2. Vipekecha shina wa mahindi (Busseola fusca; Chilo and Sesamia species)
Vipekecha shina wa mahindi ni wadudu waharibifu wa mahindi, mtama na mazao mengine katika nchi nyingi za Afrika. Viwavi wa nondo, huchimba na kuingia ndani ya shina la mahindi, wakila tishu za ndani na kusababisha mmea kunyauka na hatimaye kufa.
Wadudu hao wanaweza kudhibitiwa kwa njia mbalimbali kama mbinu za kitamaduni, hasa, kilimo cha mseto na mfumo wa ‘sukuma-vuta’ (‘pushpull’). Pia wanaweza kudhibitiwa na dawa za kuua wadudu, unga wa mwarobaini, lakini katika hatua za mapema, kabla ya mabuu kuchimba na kuingia ndani ya shina.

3. Osama/Dumuzi (Prostephanus truncates)
Dumuzi ‘Osama’ ni mdudu hatari sana wa mahindi ya kuhifadhiwa kote barani Afrika. Osama hula ndani ya nafaka na kuacha shimo na ganda tupu. Ghala safi ya kuhifadhia ni muhimu ili kuweza kuzuia uharibifu wa osama. Kukoboa nafaka kutoka kwa gunzi kabla ya kuhifadhi na kuvuna kwa wakati kunaweza kupunguza uharibifu. 

4. Funza wa vitumba (Helicoverpa armigera)
Funza wa vitumba ni mdudu msumbufu wa mimea mingi muhimu ya chakula, mafuta na fedha duniani kote, ikiwa ni pamoja na nafaka mfano Mahindi ikiwa ni mojawapo, mikunde,
matunda na mboga. Ushambulizi mkali wa viwavi wa nondo huyu kunaweza kusababisha hasara kwa mavuno yote.
Kudhibiti kwa njia ya kemikali kunapaswa kufanywa kwa makini na wakati mwafaka kwa kuwa viwavi hutoboa na kuingia ndani ya nafaka au matunda ya mmea, hivyo kuweza kulindwa. Usugu kwa dawa, kama vile za pyrethroid, kumeripotiwa katika nchi nyingi.
Bakteria aina ya Bacillus thuringiensis (Bt) na madawa ya mwarobaini hutoa udhibiti wa ufanisi dhidi ya viwavi na wakati huo huo kupunguza uharibifu wa maadui wa kiasili.
Udhibiti muhimu wa kitamaduni ni pamoja na kuondoa na kuharibu mabaki ya mimea baada ya kuvuna, kulima udongo ili uwatoe nje pupae na kupanda kwa wakati mmoja.MAGONJWA

1. Doa jani la kijivu la mahindi (Cercospora zeae-maydis & Cercospora zeina)
Doa jani la kijivu la mahindi umeibuka kama ugonjwa ulioweka kikwazo kwa mazao ya mahindi nchini Marekani na kusini mwa Afrika katika miaka 25 iliyopita. Ingawa ulidhaniwa kuwa aina moja ya kuvu, Cercospora zeae-maydis, ukaguzi wa chembechembe umeonyesha kuwa kuvu lingine, C. zeina, hupatikana kwa wingi mashariki mwa Marekani na kusini mwa Afrika. Mbegu za kuvu, zinazoishi katika mabaki ya mazao ya awali, hurushwa na matone ya mvua kwenye majani ya chini ya mmea na kusababisha madoa
marefu yanayoungana kwenye mimea isiyohimili na kusababisha baka. Mashina hudhoofika na kuanguka wakati wa mikurupuko ya magonjwa.
Ugonjwa unaweza kusimamiwa kwa kuharibu mabaki ya mimea baada ya kuvuna, kilimo cha mzunguko, kwa kutumia aina zinazovumilia ugonjwa zaidi, na, matumizi ya dawa za kuua kuvu ikiwa zitaleta faida kiuchumi.

2. Muozo wa mahindi na mycotoxin (Fusarium and Aspergillus species)
Kuna aina nyingi za kuvu zinazotokea kwenye mahindi na kuzalisha sumu za kikemikali ambazo huchafua chakula na lishe. Zinajulikana kwa pamoja kama mycotoxins, na sumu hizi zina madhara makubwa kwa afya ya binadamu na wanyama.
Aspergillus inasemekana kuwa mzalishaji muhimu zaidi wa mycotoxin katika Afrika, ingawa kuvu nyingine kama vile Fusarium pia inahusika. Makundi yote mawili ya kuvu
hukua kwenye sehemu za mimea zilizokufa na zinazooza na kusababisha kuoza kwa
mahindi katika shamba. Huzalisha unga mwingi wenye mbegu za kuvu juu ya mahindi, kabla na baada ya kuvuna, lakini pia inaweza kuwa bila kuzalisha koga lolote. Muozo wa mahindi unaosababishwa na kuvu zinazozalisha mycotoxin hutokea kwa wingi zaidi wakati mahindi yana matatizo na yanakua vibaya.
Udhibiti bora zaidi wa kuvu hizi huchanganya kuvuna kwa wakati muafaka na kukausha mahindi kabla ya kuyahifadhi. Aflasafe™, njia mpya ya kibiolojia ya kudhibiti Aspergillus, inatumika katika mashamba kabla ya mahindi kutoa maua na imeonyesha matumaini
makubwa katika kupunguza uchafuzi wa mahindi kabla ya kuvuna na baadaye mkusanyiko wa mycotoxins katika bidhaa zilizohifadhiwa.

3. Ugonjwa wa maize lethal necrosis (Multiple virus infections)
Maize lethal necrosis disease (MLND) ni ugonjwa mpya wa virusi barani Afrika.
Umesababisha wasiwasi mkubwa kwa sababu mimea hufa na hakuna nafaka au ni nafaka
kidogo tu zinazozaliwa.
Chanzo cha ugonjwa
Wataalamu katika tafiti zao wanasema kuwa, ugonjwa huu husababishwa na virusi vya aina
mbili vinavyoathiri mmea wa mahindi kwa pamoja ambavyo ni Maize Chlorotic Mottle
Virus (MCMV) na Sugarcane Mosaic Virus (SCMV).
Virusi hivi husambazwa na wadudu wa aina mbili, ambao ni Thrips pamoja na Aphids, japo
kuna wadudu wengine wanaweza kubeba na kusambaza ugonjwa huo kama vile beetles
and leafhoppers pamoja na matumizi ya mbegu zilizoathirika.
 Dalili za mahindi yalioathirika
 Majani machanga ya juu hugeuka na kuwa na rangi ya njano na hatimaye kukauka
kuanzia pembezoni mwa jani kuelekea katikati na hatimaye mmea kufa.
 Mmea huweza kutoa machipukizi mengi sana.
 Mbelewele hukosa chamvua hivyo mmea kutozaa.
 Mahindi yakishambuliwa wakati yanajaza mbegu, gunzi husinyaa na kuweka mbegu
chache au kutojaza kabisa.
 Mahindi yaliyoathirika hushambuliwa na magonjwa nyemelezi hasa ukungu.
 Kwa mimea iliyoanza kusinyaa, huonyesha dalili za kukomaa kabla ya wakati, huku
hindi likiwa katika hali ya kuchoma maganda na kuonesha utayari wa kuvunwa.
Aidha, ugonjwa huo unaposhambulia katika hindi lililokomaa, basi huingia moja
kwa moja katika kiini cha punje.
Mahindi yaliyoathiriwa na ugonjwa huu huota fangas ambayo wataalamu wanasema
ina sumu kali ijulikanayo kama Aflatoxin. Sumu hiyo, husababisha madhara kwa
binadamu na wanyama.

Utafiti uliofanywa na wataalamu mbalimbali wakiwepo wataalamu kutoka Taasisi ya utafiti wa Kilimo ya Seliani (SARI) wamebaini kuwa, sumu hiyo (Aflatoxin) inayotokana na fangasi, husababisha ugonjwa wa saratani ya ini kwa binadamu na wanyama. Utafiti huo
pia unaeleza kuwa, ugonjwa huo unaweza usionekane kwa haraka na huweza hata kuchukua muda wa mwaka ndipo kujitokeza.
Hivyo basi, ni lazima mataifa yote kuwa makini na kuchukulia jambo hili kwa uzito zaidi.

Mbinu za kuepuka ugonjwa huu
• Panda mbegu bora zilizothibitishwa na Taasisi ya Uthibiti wa Ubora wa Mbegu (TOSCI) nchini.
• Usipande mbegu zilizovunwa msimu uliopita kutoka katika shamba lililoshambuliwa na ugonjwa.
• Safisha shamba kwa kuondoa magugu na masalia yote ya mazao na kuyachoma/kuyafukia kuepuka maficho ya wadudu na virusi vya ugonjwa. Kagua shamba mara kwa mara na kama utaona dalili zilizotajwa hapo juu, toa taarifa kwa mtaalamu wa kilimo aliye karibu nawe.

Namna ya kudhibiti
• Ng’oa mapema mahindi yote yaliyoathirika, na kuyateketeza haraka.
• Usipande mahindi katika shamba lililoathirika angalau kwa msimu mmoja. Panda mazao mengine kama vile viazi mviringo, mihogo kama utakavyoshauriwa na mtaalamu wa kilimo.
• Katika maeneo yenye ugonjwa, dhibiti wadudu wasambazao ugonjwa huo kwa kunyunyizia kiuatilifu kulingana na maelekezo ya mtaalamu.
• Zingatia kilimo cha mzunguko wa mazao na toa taarifa mapema kwa afisa ugani wa kilimo endapo utaona dalili za ugonjwa.Ugonjwa wa MLND bado unafanyiwa utafiti kwa undani zaidi na dawa bado haijapatikana.
Hivyo wakulima wote wanatakiwa pindi wanapoona kuna dalili zozote zimeanza kujitokeza katika mashamba yao, hawana budi kung’oa mimea yote bila kujali kama mengine hayajaambukizwa kasha waziteketeze kwa moto. Hii ni kutokana na sababu kuwa hata mimea ambayo bado haijaonesha dalili za kuambukizwa, hana budi kuonesha dalili mapema kwani maambukizi husambaa kwa kasi sana na kwa muda mfupi.

4. Ugonjwa wa matupa kwenye mahindi (SMUT).
Ugonjwa huu hushambulia sehemu za uzazi za mahindi. Mashambulizi hufanywa na aina mbili za vimelea jamii ya uyoga (ukungu) vijulikanavyo kwa majina ya kitaalamu kama Sphacelotheca reliana na Ustilago maydis. Vimelea hivyo husababisha magonjwa ya aina mbili ambayo dalili zake zinafanana. Mimea iliyoshambuliwa na ugonjwa huu ama haizai kabisa ama inazaa kiasi kidogo ukilinganisha na jinsi ambavyo ingeweza kuzaa kama isingekuwa imeshambuliwa. Kwa hiyo mashambulizi ya magonjwa haya husababisha hasara ya mavuno. Inakadiriwa kwamba hasara ya mavuno inawezakuwa kidogo tu ama asilimia kumi (10%) au hata zaidi ya kiwango hicho, lakini kupoteza ni kupoteza hata kama ni kiwango kidogo. Ugonjwa wa "matupa" unaosababishwa na kimelea kijulikanacho kama Ustilago maydis hufahamika kama "Common Smut" kwa kiingereza.
Dalili zake huwa kuota kwa uvimbe katika sehemu za mmea zinazokua kama vile punje za mahindi, mbelewele na hata kwenye majani. Uvimbe huo ukikauka na kupasuka hutoa vumbi jeusi kama masizi ambayo ndiyo viini vya/mbegu ya huo ugonjwa. Dalili ya msingi ya ugonjwa huu kwenye mhindi ni kwamba inawezekana kuwa na baadhi ya punje zilizoshambuliwa na zingine ambazo hazina dalili katika gunzi moja.
Ugonjwa wa "smut" unaosababishwa na kimelea kijulikanacho kwa jina Sphacelotheca reliana hufahamika kama "Head smut" kwa kiingereza. Kama ilivyo kwa ugonjwa wa "smut" ya kawaida, dalili za ugonjwa huu hujitokeza mara nyingi katika hindi lenyewe na mbelewele na mara chache katika shina la mhindi. Tofauti na ugonjwa wa "smut" ya kawaida, katika ugonjwa huu badala ya mhindi kuathiriwa baadhi ya punje, hindi zima hujaa vumbi jeusi ndani ambapo kwa nje ni kama mfuko mweupe ambao kabla ya kukauka hufana na uyoga. Vumbi hilo jeusi ndilo viini vya kimelea. Vivyo hivyo kwenye mbelewele.
Wakati mwingine mmea ulioshambuliwa na ugonjwa huu hudumaa na hushindwa kuzaa.Dalili nyingine ya ugonjwa huu ni mhindi kuotesha vijani vidogo badala ya mbelewele.

UDHIBITI WA MAGONJWA YA"SMUT"
1. Tumia mbegu bora ingawa mpaka sasa haipo mbegu maalumu yenye kustahimili ugonjwa huu. Kwa kutumia mbegu bora, mkulima utajihakikishia mavuno bora.
k
2. Daima hakikisha unalima kilimo cha kisasa kikijumuisha urutubishaji wa udongo. Epuka kuijeruhi mimea uwapo shambani. Mimea iliyo na majeraha hushambuliwa kwa urahisi na ugonjwa huu. Pia dhibiti wadudu waharibifu ambao pamoja na madhara mengine wanayosababisha pia huijeruhi mimea na kwa hivyo kurahisisha maambukizo ya ugonjwa huu wa "smut".
3. Kila inapowezekana tumia kilimo cha kubadilisha mazao. Katika kubadilisha mazao ni vema kutumia mzunguko wa mazao yasiyoshambuliwa na ugonjwa wa "smut" kama vile ngano, shayiri, njegere, viazi na maharagwe.
4. Unapolima hakikisha masalia mabua yamefukiwa chini sana.

Green Agriculture Co., Ltd.
k
Green Agriculture Company
lupembe@ymail.com

+255 692 233441/+255 717 316354

Saturday, 3 March 2018

UUZALISHAJI WA ZAO LA VIAZI MVIRINGO

BIASHARA YAKE NA SOKO

Viazi mviringo ni moja kati ya zao ambalo kamwe uhitaji wake hauwezi kupungua bali unazidi kuongezeka kadiri siku zinavyokwenda na kwa umaarufu wake kutumika kupika mapishi mbalimbali ya majumbani na mahotelini.biashara ya viazi aka chips inalipa sana sio kwa mkulima tuu bali hata mpishi au muuzaji wa vyakula. sokoni kariakoo kilo moja ya viazi ni kati ya shilingi 1300-1500 (Kariakoo market cooperation) na kwa mikoani ni kati ya shilingi 800-1000. Kwa hiyo kwa mkulima mdogo wa hekari moja anaweza kupata faida ya kuazia milioni tatu na kuendelea kwa msimu mmoja (3,000,000/=)

I. UTANGULIZI:
Viazi mviringo au kwa jina jingine viazi ulaya ni jina ambalo hutumika kutofautisha zao hili na zao la viazi vitamu. Zao hili ni muhimu kati ya mazao ya mizizi katika maeneo ya miinuko ya Afrika mashariki.

Katika maeneo ya miinuko zaidi, zao hili huwa na mavuno makubwa zaidi kwa zao la mahindi na hukua kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Viazi mviringo hutumika sana kama zao kuu la chakula hapa nchini na pia husafirishwa katika maeneo ya mbali kama vila Kampala, Mombasa na Dar,es salaam.

Hapa Tanzania viazi mviringo kuzalizwa katika maeneo yenye miinuko ya kaskazini kama vile Moshi, Arusha, Lushoto na meneo ya kusini yenye miinuko kama vile Njombe mkoani Iringa na wilaya za mkoa wa Mbeya.Pia maeneo ya Morogoro yenye miiunuko hususani Tarafa ya Mgeta yameonekana kuweza kuzalisha zao hili kwa wingi.

II. MMEA WA KIAZI ULIVYO


Kiazi ni mzizi wa mmea unaovimba ukiwa chini ya ardhi na kuwa na vijicho vingi, ambavyo baada ya miezi 2 – 3 vijicho hivi huchipua na kuota shina, kijicho kimoja huweza kutoa zaidi ya shina 1 ambapo hutoa vitawi vingine.

Pingili zilizopo kwenye shina hutoa mizizi inayomea chni ya ardhi na miisho yake huvimba na kuwa kiazi. Viazi nyenye ngozi nyeupe huwa na maua meupe na ileyenye rangi hutoa maua ya rangi aidha pinki, bluuau zambarau.Katika mzunguko wa ukuaji kiazi huendelea kukua hata baada ya maua kutoka; ili mradi kuwe na na unyevunyevu wa kutosha kwenye udongo na yasiwepo magonjwa.

II. HALI YA HEWA

Mvua:-
Viazi huhitaji mvua za kiasi cha sentimita 25 kwa wiki ambazo hutakiwa kuendela kwa muda wa miezi 3 .5 hii huweza kukuza viazi na kupata mavuno mazuri.

Joto:-
Viazi hukua vizuri zaidi kwenye baridi kwa mwinuko wa mita 1,800 kulikoni kwenye joto. Maeneo machache ya mwinuko wa mita 1,500 huweza kukuza viazi, japo pia hukua kwenye mwinuko wa mita 2,900.
Udongo:-

Viazi hutoa mavuno mazuri kwenye udongo usiokuwa mzito na unaopitisha maji kwa urahisi. Udongo wenye viini lishe vya kutosha au kuongeza samadi na mbolea za viwandani.

IV. AINA ZA VIAZI

Aina zote za viazi zimeingizwa Afrika Mashariki kutoka Ulaya ambako huzalishwa kwa wingi.

Dutch Robijn - kutoka Holland

- ndani ni njano
- inavumilia kidogo ugonjwa wa ukungu
- hushambuliwa sana na Mnyauko Bakteria
- hupendwa na walaji wengi

ii. Roslin - kutoka Scotlland

- ngozi yake ni nyeupe
- ndani ni nyeupe
- huvumulia ugonjwa wa ukungu

iii. Kerr’s Pink - 

ngozi yake ni nyeupe au nyekundu
- ndani ni nyeupe
- hushambuliwa sana na ukungu na Mnyauko Bakteria

iv. Atzimba - kutoka Mexico
- huvumilia ugonjwa wa ukungu

V. MBEGU ZAKUZALISHA VIAZI
Viazi vyenye umbile dogo hutumika kama mbegu, hutakiwa kuwa na upana wa sentimita 3 – 6. Kiasi cha robo tatu za tani huhitajika kuotesha ekari 1 sawa na tani 1.85 kwa hekta 1.
Mbegu hazitakiwi kuhifadhiwa kwenye giza nene kwani zitaanza kutoa vichipukizi virefu vyeupe.

VI. KUANDAA SHAMBA
Shamba linatakiwa kuandaliwa vituta vidogo vidogo kwa nafasi ya sentimita 75 kutoka tuta hadi tuta, hiihusaidia kuhifadhi udongo na maji na hutoa nafasi nzuri wakati wa upanukaji wa viazi.
Inashauriwa pia kama matuta hayajatumika basi ni muhimu kujaza udongo kwenye shina kwani pingili za chini kwenye shina ni lazima zifunikwe na udongo ili zitoe viazi kwa wingi na hivyo mavuno huongezeka.

VII. KUOTESHA VIAZI

Viazi hutakiwa kuoteshwa mara karibu kabisa na mvua zinapotaka kuanza kuchelewa kuotesha kutapunguza kipindi cha ukuaji wa ile mizizi ili iwe viazi na hivyo kukabiliwa na kipindi cha ukavu.

Uoteshaji hufanyika kwa mikono na mbegu ziwekwe chini udongo kwa kina cha sentimita 10. Kama mbegu zitaoteshwa bila matuta basi zioteshwe kwa kina cha sentimita 15 na kufunikwa na udongo mchache na wakati wa palizi udongo utaongezwa ili kuongeza utoaji wa viazi kwa wingi. Nafasi ya kuotesha ni sentimita 75 toka mstari hadi mstari na sentimita 23 – 30kwa mche hadi mche.

VIII. MBOLEA

Viazi hustawi vizuri zidi kwenye udongo ulioongezwa samadi na ni muhimu chimbiwe katika kina kirefu. Mbolea za viwandani zinazotakiwa ni zile zenye Nitrogeni kwa kiasi cha kilo 22 – 45 kwa ekari; zenye Chokaa P2O5 kwakilo 45 – 65 kwa ekari.

Ni vyema kuongeza mbolea na samadi wakati kuna mategemeo mazuri ya mavuno kwa kuzingatia kuwa mbegu zilizooteshwa hazina magonjwa ya aina yoyote.

IX. PALIZI

Zao la viazi likioteshwa kwa nafasi zilizoshauriwa basi huweza kufunika ardhi yote na hivyo kugandamiza magugu, hii husaidia kwa kipindi cha wiki 6 za mwanzo. Katika mpando wa matuta, basi huwa ni kuondoa magugu na kujaza udongo kwenye mashina.

X. KUVUNA

Uvunaji wa viazi hufanyika kwa kutumia jembe la mkono, viazi vikishang’olewa kutoka chini ya udongo visiachwe kwa muda mrefu kwani vitabadilika rangi na kuwa kijani.

Ili kuifanya ngozi yaviazi kuwa ngumu na isiharibike kirahisi basi mashina yote yanyofolewe wiki 2 – 3 kabla ya kuvuta viazi juu ya udongo. Baada ya viazi kuvunwa haviwezi kuhifadhiwa kwa muda mrefu kwani huanza kuchipua. Viazi huweza kuhifadhiwa kwenye ardhi, lakini si zaidi ya wiki 6 kwani vitakabiliwa na magonjwa na kushambuliwa na minyoo fundo.

XI. MAVUNO

Mavuno huwa mengi kama utunzaji wa kitaalamu umezingatiwa ikiwa ni pamoja na kudhibiti magonjwa, kutumia aina zinazostahimili magonjwa. Kiasi cha tani 6 – 8 kwa ekari huvunwa,sawa na tani 15 – 20 kwa hekta.

KUHIFADHI:-
Uhifadhi wa zao hili ni mgumu, hivyo inashauriwa kuwa sehemu iliyotengwa kwa biashara iuzwe mapema, sehemu ya kutumia nyumbani ihifadhiwe katika banda au ghala safi lenye sakafu, lisilo na unyevu, mwanga wala joto- liwe na hewa safi na ya kutosha. Vinginevyo husababisha viazi kuota haraka. Viazi vilivyowekwa ghalani visilundikwe kwa kina kirefu, visambazwe ili visipate joto.

XII. WADUDU

Vidukari:-
Ni wadudu wadogo wanoshambilia majani na mashina kwa:
- kufyonza utomvu na kusababisha kunyauka kwa mmea.
- Majani kujikunja kuelekea juu.
- Majani kuwa magumu
- Mimea kudumaa
- Pia hubeba vimelea aina ya virusi ambao huathiri mimea.
- Pia hueneza ugonjwa wa virus.

Tiba:- Wakati wa utunzaji wa mbegu za viazi ni muhimu kupiga dawa ya wadudu ili kuepuka kupuliza shambani kwani dawa nyingi itapotea.

Nondo wa viazi:-
Wadudu huathiri viazi vilivyooteshwa wakati ambao sio wa msimu wa viazi. Viwavi wanaoanguliwa huingia ndani ya viazi na kusababisha kuoza. Pia huingia ndani ya viazi wakati vikiwa stoo.

Kuzuia:-
- Otesha viazi katika kinachoshauriwa au zaidi ya sentimita 3 kwani kiwavi
aingiae ndani ya hawezi kuchimba kina kirefu na inulia matuta wakati viazi vinakuwa, hii husaidia kuzuia nondo kutaga mayai.

- Viazi vyote vilivyochimbwa ni muhimu viwekwe kwenye mifuko na mapema kabla ya alasiri ili kuepuka nondo kutaga mayai.
- Vikihifadhiwa stoo majani ya aina ya LANTANA CAMARA yaweza kutumika.
-
Tiba:- Wakati viazi vikiwa stoo, dawa ya unga ya Aldrin hutumika kwenye viazi vya mbegu.
Nyunyizia majani ya viazi wakati mmea ukiwa na mwezi 1dawa aina ya Dipterex, Diazon, Thiodan, Permethrin, ACtellic au Sumithion.
Kama ni viazi vya kula basi tumia PYRETHRUM.

Minyoofundoo:-

Hushambulia viazi vilivyoachwa kwa muda mrefu ardhini na kwenye ardhi iliyoathirika na mmomonyoko.

Kuzuia:-

- Usioteshe mbegu ambazo zimeshambuliwa na wadudu.
- Andaa shamba mapema ili masalia yote ya mazao yaweze kuoza ili
kutoruhusu makazi ya minyoo fundo.

Mbawakavu:-

Ni wadudu wadogo ambao hutafuna majani na kuacha matundu matundu.

Kuzuia: Tumia dawa aina ya Malathion, Thiodan

MUHIMU:-
Pamoja madhara ya wadudu pia hueneza magonjwa mbali mbali ya mimea, hivyo kutunza shamba kuwa safi hasa kupalilia; kuchimba na kutupa mbali maotea pamoja na masalia yote na kubadilisha viazi na vipando kama maharage, mahindi, hupunguza madhara.ZALISHAJI WA ZAO LA VIAZI MVIRINGO


Thursday, 2 November 2017


FAHAMU NAMNA NZURI YA KUVUNA MAJI YA MVUA
Eng Octavian Justine Lasway
Irrigation and Water Resources Engineer
Sokoine University of Agriculture
Green Agriculture Company Limited 
0763347985/0673000103
Wasiliana na nasi kwa ajili ya usanifu,utengenezaji na ununuzi wa materials 

Katika maeneo mengi ya Afrika mashariki hususani Tanzania tuna kiasi  kikubwa sana cha maji kwenye mito, chemichemi, maziwa na maji ya ardhini(undergroundwater) ambapo asilimia 70% hutumika kwenye kilimo kwa kuzalisha mazao mbalimbali

Tuesday, 29 August 2017

JIFUNZE KILIMO CHA KUNDE


Mkulima Mama Angela Machibya akiwa shambani kwake Tanga , akivuna Choroko

UTANGULIZI
Kunde ni zao ambalo linaweza kulimwa kwa ajili
ya chakula na bishara ni zoa lenye kiasi
kukubwa cha protini na majani yake yanaweza
kutumika kama mboga za majani.Ni zao ambalo
linatoa mavuno ya Kiasi cha kilogram 500 hadi
1500 kwa ekari.

HALI YA HEWA IFAAYO
Ni zao linalostahimili ukame, Kunde hukubali
vizuri katika mwinuko wa mita 0 hadi 1500
kutoka usawa wa bahari.kunde huweza kulimwa
katika maeneo yapatayo mvua kidogo kiasi cha
milimita 500 hadi 1200 kwa mwaka.Hukuwa
vizuri katika joto la nyuzi 28 had 32 C

ARDHI IFAAYO KWA KILIMO CHA KUNDE

Huweza kulimwa katika udongo usiotuamisha
maji wa aina tofauti tofauti kuanzia kichanga
hadi mfinyazi.Zinaweza kupandwa katika
udongo usio na rutuba ya kutosha lakini hustawi
vizuri katika udongo wa tifutifu kichanga au
tifutifu mfinyanzi au  mchanganyiko wa mfinyazi
na kichanga wenye p.H kati ya 6 hadi 7, ni vizuri kupima udongo kwa ajili ya uhakika zaidi

MAANDALIZI YA SHAMBA LA KUPANDA KUNDE


Shamba la kunde liandaliwe mapema kabla
shughuli ya upandaji kuanza, Kama ni la kukata
miti mikubwa miti ikatwe mapema,Kama ni la
kufyeka nyasi na miti midogo shughuli hii
ifanyike mapema kabla hatua ya kulimwa kwa
shamba kwa kutumia trekta,Pawatilla,jembe la
ng'ombe au la mikono.shamba lisawazishwe na
kukusanywa mabaki ya mimea au visiki na
mawe madogomadogo kama yapo.

MBEGU BORA ZA KUNDE

Kuna aina mbalimbali za mbegu bora za kunde
ambazo zimegawanyika katika makundi
makubwa mawili.Kunde zinazosimama na kunde
zinazotambaa.

BAADHI YA MBEGU BORA NA SIFA ZAKE
1.TUMAINI
Hukomaa kwa muda wa siku 75 – 90. Aina hii ya
kunde husambaa ina maua yenye rangi za
zambarau na mbegu zake ni mviringo. Maeneo
yanayoshauriwa kupanda ni yenye mwinuko wa
mita 0 – 1500 toka usawa wa bahari. Inahitaji
udongo mwepesi wenye rutuba na usiotuamisha
maji. Kunde hizi hutoa mazao hadi tani 3
(kilogram 600 - 1500 kwa ekari)kwa hekta moja.
Huvumilia virusi vya mozaiki vinavyotokana na
wadudu mafuta wa kunde na bakteria. Aina hii
ya kunde ilizalishwa mwaka 1992 na Kituoa cha
Utafiti cha Ilonga kwa ushirikiano na Naliendele.

  2.FAHARI
Aina hii hukomaa kwa siku kati ya 75 – 90.
Mmea husambaa na maua yana rangi ya
zambarau. Mbegu zake ni za mviringo. Hustawi
maeneo yenye mwinuko wa mita 0 – 1500
kutoka usawa wa bahari. Hutoa hadi tani 3 kwa
hekta moja (kilogram 600 - 1500 kwa ekari ).
Huvumilia magonjwa ya CABMV na mabaka.
Fahari ilitolewa mwaka 1982 na Kituo cha Utafiti
Ilonga kwa kushirikiana na Naliendele

  3.VULI_1
Inakomaa kwa siku 55 – 65. Hukua ka kunyooka
na kusambaa kidogo. Mbegu zake ni nyekundu
na za mviringo. Inastawi vizuri maeneo yenye
mwinuko wa mita 0 – 1500 toka usawa wa
bahari. Ikipataiwa matunzo mazuri huto hadi tani
2 kwa hekta moja (Kilogram 450-800 kwa ekari).
Vuli – 1 inavumilia CABMV, BP na BB Vuli – 1
ilizalishwa mwaka 1987 kutoka kituo cha utafiti
Ilonga.

4.VULI_2
Inakomaa baada ya siku 65 – 70 baada ya
kupandwa inaota ikiwa imenyooka na kusambaa
kidogo. Mbegu zake zina weupe uliofifia na ni
mviringo. Aina hii husitawi vizuri maeneo yenye
mwinuko wa mita 0 – 1500 kutoka usawa wa
bahari. Katika matunzo mazuri aina hii huzalisha
hadi tani 3.5 kwa hekta moja(Kilogram 800
-1200 kwa ekari) . Vuli – 2 huvumilia CABMV, BP
na BB Vuli – 2 ilizalishwa mwaka 1987 kutoka
kituo cha utafiti Ilonga.


KUPANDA KUNDE

Kunde hupandwa mwishoni mwa msimu wa
mvua ili kuziepusha kukauka wakati mvua
inaendelea kunyesha.na pia unweza kupanda
wakati zao jingine linakaribia kuvunwa au katika
shamba lilivunwampunga na lina unyevu wa
kutosha.Muda mzuri wa kupanda kunde ni
akuanzia mwezi Februari mwishoni hadi Machi
na Aprili kwa maeneo ambayo mvua huchelewa
kuisha.
  KUMBUKA; Mbegu zinazotambaa za
kunde zipandwe miezi miwili kabla ya mvua
kuisha kwani hizi huchukua siku nyingi kukomaa
na Mbegu zinazosimama zipandwe mwezi
mmoja kabla ya mvua kuisha.
Kunde huitaji kiasi cha kilogram 4-12 za mbegu
kwa ekari.kiasi cha mbegu kitategemea ukubwa
wa mbegu,(mbegu kubwa zitahitajika kilogram
nyingi) nafasi za upandaji,Ukipanda karibu
karibu na mbegu itahitajika nyingi,Ubora wa
mbegu katika uhotaji.Zisizoota vizuri huitaji
mbegu nyingi zaidi


NAFASI YA UPANDAJI

Unaweza kutumia nafasi zifuatazo kwa kupanda
kunde zako
KUNDE ZINASOSIMAMA-Tumia sentimeta 45
hadi 50 mstari hadi msatari na sentimeta 15 hadi
20 shina hadi shina katika mstari / Sm
 ( 50 X20 )

KUNDE ZINAZOSAMBAA-
Tumia nafasi ya Sentimeta 70 hadi 75 mstari hadi mstari Kwa sentimeta 25 hadi 30 shina hadi shina katika mstari / Sm ( 75 X 30 )
Panda kwa kufikia kiasi cha sentimeta 2.5 hadi 5
ardhini na tumia mbegu tatu kwa kila shimo na
baadaye punguza uache 2 kwa kila shimo kama
unauhakika wa mbegu zako unaweza kupanda
moja kwa moja mbili mbili kwa shimo

PALIZI NA KUPUNGUZA MIMEA      KATIKAMISTARI

Palilia na Punguza mimea mapema katika
shamba lako la kunde.ili ikuwe ikiwa na afya
bora.

MBOLEA YA SAMADI NA MBOLEA ZA VIWANDANI

Kama shamba lako halina rutuba ya kutosha
unaweza kuongeza samadi kiasi cha tani tano
kwa ekari moja na uhakikishe mbolea hii
imemwagiwa au imenyeshewa na mvua ya
kutosha kuiozesha kabla ya kupanda kunde
zako na pia unaweza kupanda kwa kutumia
mbolea ya TSP kiasi cha Kg 50 kwa ekari na
baadaye kukuzia mbolea ya SA kiasi cha Kg 50
kwa ekari.

WADUDU NA MAGONJWA KUNDE
KUDHIBITI WADUDU WAHARIBIFU WA KUNDE

Wadudu waharibifu wa zao la Kunde wako katika
makundi mawili:-
     1. Kundi la kwanza ni la wadudu
wanaoshambulia mimea ikiwa shambani.
 Inamaana mmea hushambuliwa baada ya kuona
hali inapokomaa na kutoa mbegu. Kundi la
wadudu hawa lina tabia ya kufyonza (Sap =
supu) ya mmea kwenye majani, matawi,
mashina, maua hata mbegu hasa zikiwa changa
kama vitunda. Njia hii ndiyo pekee kwa wadudu
wa kundi hili kujipatia mlo ili waishi na
kuzaliana. Katika kundi la pili kuna wadudu
wenye tabia ya kukata mashina na kuangusha
mimea michanga na wengine hutafuna majani
na maua. Zaidi ya uharibifu katika kula mimea,
wadudu wengi ni hifadhi ya viini vya magonjwa
ya virusi.

 2.Kundi la pili ni la wadudu waharibifu baada
ya mavuno kuwekwa ghalani.
 Athari ya wadudu hawa inapelekea wakulima kupoteza chakula
ghalani pia kupunguza chakula ghalani pia
kupunguza ubora wa mazao yanapopelekwa
sokoni mfano Mahindi yanapofunguliwa soko
lake ni duni. Jamii za wadudu na athari zao
zinaelezwa katika aya zifuatazo:-

1. KUNDE:
(ii) Foliage beetle (Ootherca mutabilis)
Wadudu hawa hushambulia mimea ya kunde
baada ya mbegu kuota (Seedling stage). Wakiwa
kwenye hatua ya mdudu kamili (adult stage)
hushambulia majani kwa kula sehemu kati ya
vihimili vya majani (area between leaf veins).
Mashambulizi ya wadudu wengi husababisha
mmea kupoteza majani yote na hatimaye mmea
kufa.
Kuzuia jamii ya wadudu hawa:
Dawa za chemikali aina ya endosulfan, Karate
n.k. huagamiza mashambulizi kwa mpulizo
mmoja.
(i) Aphids (Aphis gaccivora)
Hawa ni kati ya wadudu wenye kusababisha
hasara kubwa katika zao la kunde.
Wanapendelea kula mvunga wa majani (under
leaf), sehemu za vishina na hata vitumba (pools)
vya mbegu. Athari za mashambulizi: Mmea
hudumaa, majani husinyaa na kukunjamana pia
hupukutika kabla hayajazeeka hatimaye mmea
hufa.
Kuzuia Aphids: Dawa za kemikali aina ya
phosphomiolon na dimethoate kwa cc 40 katika
lita 10 za maji.
(ii) Flower thrips (Megalurothrips sjostedti)
Hatua ya mdudu kamili hushambulia maua.
Mimea ikishambuliwa sana haizai matunda
kwasababu maua yameharibika. Mashambulizi
yakiwa makubwa zao lote huangamia.
Kuzuia: Kwa kutumia chemikali aina ya
Cypermethrin – kiwango cha cc 40 katika lita 10
za maji.
(iii) Podborers (Maruca testulalis)
Wadudu hawa hula mvungu wa majani, ganda la
shina na vitumba vya mbegu katika hatua ya
kukomaa. Athari: Mmea hudumaa, umbo la
majani huharibika (olistorted leaves) na
hupukutika kabla ya kuzeeka. Mimea mingi hasa
michanga hufa.
Uzuiaji: Kwa kutumia chemikali aina ya
phosphomidon na dimethoate kwa kiwango cha
cc 40 katika lita 10 za maji.
(iv) Podsucking bugs (Anoplemenia,dentires,
Acanthomia SPP)
Wadudu hawa hushambulia mikunde katika
hatua ya kuweka vitumba (pods). Hasara,
inayosababishwa, na wadudu hawa hufikia 90%.
Madhara makubwa huletwa na hatua ya wadudu
kamili (adult stage/ kwa kufyonza “Sap = Supu”
ya vitumba teketeke ambavyo husinyaa na
kukauka bila kukomaa wala kuwa na mbegu.
Kuzuia: Kwa kutumia chemikali za Endosulfan au
dimethoate kwa kiwango cha cc 40 katika lita 10
za maji.
(v) Cowpea storage weevils (Callosobrunchus
macuhates callosobrun ams chinensis).
www.kilimofaida.blogspot.com
Mashambulizi ya wadudu hawa wawili huanzia
shambani wakati kunde zimekaribia kukomaa.
Wadudu hutaga mayai kwenye vitumba
vilivyokomaa. Mayai yakiangauliwa, funza
hupenya kupitia kwenye matobo
yanayosababishwa na wadudu wengine. Funza
wakianguliwa hushambulia mbegu na uharibifu
hufikia 70% ya mbegu safi.
Kuzuia: Tumia chemikali aina ya Acteric Super
Dust 100 mg za unga wa dawa katika 10 Kg za
mbegu safi (Seed grain)


NAMNA YA KUZUIA MAGONJWA YA ZAO LA
KUNDE:

Magonjwa hatari yanasababishwa na vimelea
vya virusi na vya bacteria aina tabia na uzuiaji
wa magonjwa haya ni kama ifuatavyo:-

(i) Cowper aphid-born mosaic virus
Ugonjwa huu husababishwa na virusi na
hupelekea mkulima kupata hasara ya 13 – 87%
ya zao.
Dalili za ugonjwa huu ni michirizi ya
rangi ya kijani iliyochanganyika na njano au ya
ugoro (mosaic & mottling) kwenye majani.
Kuzuia: Kwa kutumia aina za kunde zenye
kustamili ugonjwa huu kama Tumaini, Fahari na
Vuli.

(ii) Bacterial blight (Xanthomonus vignicola)
Ugonjwa huu hushambulia sana miche na kiasi
cha 60% ya miche yote hufa.
Dalili: Majani,vitumba au mashina ya mimea
iliyoathirika huwa na vidonda vyenye rangi kati
ya njano ya chungwa. Katika mashambulizi
makubwa vidonda vidogo huungana (merge –
coleasce) na eneo kubwa la majani huharibika.
Ugonjwa hushamiri katika kipindi cha mvua
nyingi (Kifuku) na umwagiliaji kwa juu (Overhead
irrigation).
Kuzuia: Tumia mbegu zinazovumilia ugonjwa
kama Tumaini, Fahari na Vuli.

(iii) Bacterial blight (Xanthomonas Spp)
Ugonjwa hushambulia aina ya kunde pori na
zinazolimwa.
Dalili: Vidonda vidogo huonekana uvunguni mwa
majani. Katika mimea dhaifu (more susceptible)
vidonda huungana na kuwa na umbo la duara
lenye ukubwa wa: kipenyo cha 1-3 cm.
Mwanzoni vidonda huonekana kufutuka
mvunguni mwa jani kadiri vinapokomaa huwa
na rangi ya kahawia upande wa juu na majani.
Baada ya muda vidonda hukauka na hubakisha
migonyeo sehemu zilizoathirika. Majani mengi
yaliyathirika hubadilika kuwa njano na baadaye
huanguka / hupukutika.
Ueneaji: Ugonjwa huenea kwa kasi wakati wa
kifuku (mvua nyingi) na umwagiliaji unapokuwa
wa juu. (overhead irrigation). Kimelea cha
bacteria huyu hudumu kwenye punje (mbegu).
Kwa hiyo mbegu za namna hii huota zikiwa na
viini vya ugonjwa.
Kuzuia: Kutumia mbegu zenye kustahimili
ugonjwa huu kama Tumaini, Fahari na Vuli

(iv)Powdery Mildew (Ukungu)
Dalili-Majani yanakuwa na vidoti vya njano
ambavyo vinabadilika kuwa vya kahawia au
kijivu haraka na ambapo kunakuwa na unga
unga katika majani.
Kinga na tiba-Panda mbegu zinazostahimili
ukungu,Pulizia dawa za ukungu (Fungicide).
anza kupuliza wiki tatu baada ya mimea kuota
na kuendelea kulingana na hali halisi ya
ugonjwa.

UVUNAJI

Vuna kunde zako baada ya kukomaa na kuanza
kukauka kwa kung'oa mashina au kuchuma kwa
mikono.Kisha zisambaze kunde zako au
mashina yako juani ili zikauke zaidi na uweze
kuziondoa kwa urahisi kutoka katika maganda
yake.
Unaweza kuondoa maganda yake kwa
mkono au kuupigapiga taratibu au kwa
kutwanga katika kinu taratibu bila kuzipasua
Kwa maelezo zaidi wasiliana nasi kwa simu namba 

Walter Emmanuel 
0718 405318
Na
Octavian Lasway 
Irrigation and water Engineer
+255763347985/673000103

YouTube


GREENAGRICULTURE APP

GREENAGRICULTURE APP
GREENAGRIC APP

Business

AGRICULTURE LAND

LIKE US ON FACEBOOK

visitors

Mostly Visited